WEMA, AUNT HESHIMA YENU IKO WAPI?

KWENU,
Wema Sepetu na Aunt Ezekiel. Wenyewe mwajiita mastaa wa Bongo. Ni kweli lakini ngoja niwaambie, ustaa ni staha! Kiukweli mnajisahau sana. Mnaamini hapo mlipo ndiyo mmefika na hakuna uwezekano wa kuporomoka!


Mnajidanganya sana, bila staha mtaporomoka. Wapo mastaa wengi tuliokuwa nao miaka ya mwanzoni mwa 2000 sasa hivi chali, lakini wapo wengine ambao wanaendelea kutesa mpaka sasa.
Ni suala la kuheshimu nafasi mliyopewa tu. Watanzania wamewaamini, wamewapokea na wamekubali kazi zenu lakini mnaharibu.
Mna heshima kubwa lakini mnaibomoa wenyewe. Ni juzi tu, mmefanya madudu tena. Mmesafiri hadi China kwa ajili ya birthday – ni sawa. Tatizo ni namna ya kuisherehekea!

Labda ni utamaduni wenu wenyewe, kupiga picha za kipuuzi kama mlizopiga lakini sasa kwa nini mzisambaze? Maana haiingii akilini kwamba zile picha zilijiingiza zenyewe kwenye mitandao.
Hata hivyo, jamii itawachukuliaje? Ndugu zenu wanajifunza nini kwa ninyi kula denda? Hizo ni tabia za Kimagharibi, hazipo kabisa katika utamaduni wetu Waafrika.
Kinachosikitisha si tukio la kwanza. Kuna kipindi mlifanya vitu vya hovyo. Mlijiachia jukwaani vibaya. Magazeti yakaandika, lakini baadaye mliita waandishi wa habari na kuomba wawafikishie ujumbe kwa Watanzania.
Mliomba radhi kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari. Naamini na ndivyo ilivyo, jamii iliwaelewa na iliwasamehe na kuwapa nafasi nyingine – leo ni yaleyale!
Jamii inawaelewaje? Ni kweli mnataka sanaa yenu iheshimike kwa staili hii? Sanaa inajengwa kwa nidhamu. Achana na mashabiki ambao labda kwenu hawana maana wala thamani lakini vipi kwa Aunt ambaye ni mke wa mtu?
Dada zangu ni vyema mkawa makini. Kuwa staa si kazi ndogo lakini kazi kubwa zaidi ni namna ya kuendelea kubaki kileleni na heshima ikiwa palepale.
Kitendo mlichokifanya ni sawa na kuwatusi Watanzania. Kuwaambia hawana lolote na si lazima washabikie kazi zenu. Ni kuwaambia kwamba, wao ni watoto wadogo ambao wanaweza kudanganywa tu!
Ni kweli, kila mtu ana uhuru wake na ana uamuzi wa kuishi apendavyo lakini yapo mambo ambayo ni mwiko kwa mila na desturi zetu ambayo yanakemewa kila siku.
Kwa ninyi ambao ni mastaa mkifanya jambo baya, jamii nzima inawaangalia. Mabinti wadogo ambao bado hawana uwezo wa kuchanganua mambo vyema, huamua kuchukua kila kinachofanywa na ninyi kama dira kwao.
Vipi, mkikutana na wadogo zenu wakiwa wanakula denda? Je, kwa mtindo huu sanaa inaweza kuheshimika au watu wataamini ni genge la wahuni tu?
Je, kwa mzazi ambaye mtoto wake analilia kila siku awe msanii, atamruhusu kwa mtindo huu? Hakuna mzazi ambaye atapenda mwanaye aishie pabaya. Kwa mtindo huu kutakuwa hakuna kizazi kijacho cha sinema.
Amini msiamini, mnajishusha thamani wenyewe. Wasanii wengine wajifunze kupitia kwenu na wasifanye madudu kama yenu. Thamani ya ustaa inalindwa na staa mwenyewe! Kazi kwenu.
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter