TAMKO LA MAHAKAMA KUU KUHUSU KESI YA KAMPUNI ZA SIMU KUPINGA KODI YA SH 1000 KWA KILA MTANZANIA...



MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana iliziruhusu kampuni tano za simu kuingia kwenye kesi ya msingi kupinga sheria ya kodi ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu.
 
Kuruhusiwa kwa kampuni hizo kulitokana na mjadala ulioibuka Oktoba 7, mwaka huu, mahakamani hapo baada ya upande wa Jamhuri kupinga kuingia kwa kampuni hizo na kuzua mjadala wa kisheria.
 
Kampuni hizo ni Vodacom, Airtel, Mic Tanzania Ltd, TTCL na Zantel ambazo zinaungana na Taasisi ya Kutetea Walaji wa Bidhaa na Huduma kuitaka Mahakama itamke kwamba sheria hiyo ni kandamizi.

Uamuzi huo ulitolewa na Mwenyekiti wa jopo la majaji watatu, Aloysius Mujulizi akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory Bongole.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kuziandikia kampuni za simu ili zianze kutoza kodi hiyo Septemba 30, 2013.
 
Baada ya uamuzi wa jopo hilo, mawakili wa upande wa walalamikaji wakiongozwa na Wakili Fatma Karume, walitakiwa kupeleka maelezo yao kwa maandishi Oktoba 15, mwaka huu iwapo watafanya marekebisho kwenye maombi ya msingi ya kesi hiyo.
 
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali , George Masaju, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Elicia Mbuya, ulikubaliana na uamuzi wa Mahakama.
 
Akiahirisha kesi hiyo, Mwenyekiti wa jopo hilo, Jaji Mujuluzi alisema kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 21, mwaka huu.
 
Katika kesi ya msingi iliyofungiliwa chini ya hati ya dharura, taasisi hiyo inadai kwamba watumiaji wengi wa simu za mkononi hawana uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi, huku wakisisitiza kuwa itawaathiri watumiaji wa huduma hiyo.
 
Sheria hiyo ilipendekezwa na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) na kupitishwa kwenye Bunge la bajeti lililotaka utekelezaji wake uanze Julai 30, mwaka huu, ili kukusanya sh bilioni 178 kwa ajili ya kusaidia shughuli za bajeti kuu ya serikali.
 
Malalamiko hayo yalimlazimu Rais Jakaya Kikwete kukutana na wadau wa mawasiliano wakiwamo mawaziri wake, kisha kuwaagiza waangalie namna ya kuziba pengo hilo iwapo kodi hiyo itaondolewa.

Licha ya agizo la rais kutekelezwa kwa wenye kampuni za simu kutakiwa kuongeza kodi nyingine iitwayo ‘Excise Duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17 bila kujali kwamba katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka asilimia 12 hadi asilimia 14, kodi ya laini za simu haijaondolewa.

Takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonesha kuwa miongoni mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini ya sh 1,000 kwa mwezi.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter