Ripoti mpya ya utafiti imebaini kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wenye elimu ya darasa la saba na wale wasiosoma, ndiyo wanaokubaliana na utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete.
Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la ‘Namna Watanzania wanavyouangalia utendaji kazi wa Bunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Asasi ya Afrobarometer, inaonyesha kuwa asilimia 77 ya waliokosa elimu ndiyo wanamuunga mkono Rais Kikwete.
Afrobarometa ni Asasi ya Kimataifa inayojumuisha taasisi tatu za Institute for Democracy ya Afrika Kusini, Ghana Centre for Democratic Development ya Ghana na Political Science Department ya Chuo Kikuu cha Michigan cha Marekani.
Mtafiti Msaidizi wa Afrobarometer, Stephen Mwombela akisoma ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema asilimia 72 ya wale walioishia darasa la saba ndiyo wanamuunga mkono Rais.
Wakati asilimia 23 ya watu wasiosoma ndiyo hawamkubali Rais na asilimia 28 ya wale walioishia darasa la saba, pia hawaridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo.
Mwombela, hata hivyo, alisema utafiti huo uliohusisha watu 2,400 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wasomi wa kiwango cha sekondari na kuendelea wanaunga pia mkono utendaji wa Rais, lakini siyo kwa kiwango cha juu kama wale ambao hawajasoma.
“Asilimia 60 ya waliosoma elimu ya sekondari na kuendelea wanaunga mkono utendaji wa Rais, lakini 40 hawakubaliani na utendaji wake,” ilisema taarifa ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Mei hadi Juni mwaka jana.
Matokeo ya utafiti huo yanatofautiana na yale ya mwaka 2008, ambayo yalionyesha kuwa wasomi walikuwa wanamuunga mkono Rais kwa asilimia 92.
Pia katika matokeo ya utafiti huo wa mwaka 2008, ulionyesha kuwa wasiosoma walimuunga mkono kiongozi huyo kwa asilimia 92.
Imani ya wananchi kwa Rais.
Ripoti hiyo ilisema pia imani ya wananchi kwa utendaji wa Rais imeshuka hadi kufikia asilimia 74 kwa mwaka jana, tofauti na asilimia 94 ya mwaka 2005 wakati aliposhika wadhifa huo.
CREDIT: MWANANCHI
CREDIT: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....