Tarehe 20/09/2013 majira ya saa 4 mpaka saa 5 usiku Huko Buhongwa mtaa wa Ihila wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza yalitokea mauaji ya watu watatu wa familia moja ambao ni James Elias (44), Lucia James (35) pamoja na mtoto wao aitwaye Eliudi James umri wa mwaka mmoja.
Mauji hayo yanasadikika kufanywa na Lameck Paul (33) mkazi wa igombe wilayani Ilemela jijini Mwanza aliyekuwa mgeni katika familia hiyo kuanzia tarehe 17/09/2013 ambaye alitoweka mara baada ya kufanya tukio hilo.
Muuaji huyo alifika nyumbani kwa marehemu tarehe 17/09/2013 ili kufanya kibarua cha kufyatua matofali kwaajili ya ujenzi wa Nyumba ya matofali na walitegemea kuianza tarehe 22/09/2013 kwa muda wa siku nne.
Muuaji huyo alielewana na marehemu James Elias kwamba ameuza kiwanja chake huko maeneo ya Buswelu na pesa hiyo alitaka kuitumia kujenga nyumba ya pili na ndio maana alimtafuta kwaajili ya kumfyatulia matofali ili apate pesa.
Muuaji alimshawishi marehemu ampe kiasi chochote cha pesa kama malipo ya awali kwenda kulipa huko Igombe alikokuwa akidaiwa fedha ambayo ilikuwa ni fidia ya mifuko miwili ya sementi aliyokuwa ameiba siku za nyuma.
Baada ya kugundua kuwa marehemu hakuwa tayari kutoa pesa aliyokuwa anahitaji, muuaji huyo alijenga dhamira ya kumuua marehemu ili achukue pesa yote.
Majira ya saa 4 na saa 5 usiku Lameck Paul alitoka nje na aliporudi alikuwa tayari amechukua shoka na kuaanza kumshambulia kichwani kwa kumkatakata kichwani na sehemu ya chini ya sikio la kushoto hali iliyosababisha mauti.
Baada ya kumuua alimuita mke wa marehemu aliyekuwa amelala chumbani na alipotokeza alimshambulia kwa shoka na kuangukia chumbani, alimfuata na kumnyonga kwa waya wa umeme.
Mauaji yaliendelea baada ya mtoto mdogo wa mwaka mmoja aliyekuwa amelala na mama yake kuanza kulia ndipo muuaji alimchukua na kumnyonga kwa kutomia waya ule ule aliomnyongea mama yake.
Polisi waliendelea kumsaka mtuhumiwa huyo na mnamo tarehe 5/10/2013 mtuhumiwa alikamatwa akiwa nyumbani kwa mganga wa kienyeji Anastazia Joseph (38), mkazi wa kijiji cha Hinduki - Malampaka wilayani Maswa ambapo alikuwa akifanyiwa zindiko ili asikamatwe.
Mtuhumiwa alikiri kufanya mauaji hayo na kuiba kiasi cha pesa Tsh. 200,000/= suruali mbili na T-shirt moja, radio ndogo nyeusi, simu mbili za mkononi aina ya Nokia na mashine ya mahesabu (Calculator).
Mtuhumiwa alirejeshwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kuonyesha shoka alilotumia kufanyia mauaji.
Mnamo tarehe 7/10/2013 majira ya saa za mchana katika maeneoya mtaa wa Ihila kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza askari wakiwa na mtuhumiwa huyo wakielekea eneo alikoficha shoka alilotumia kufanya mauaji, baada ya kufika eneo la tukio kundi la wananchi waliitokea maeneo mbalimbali wakiwa na mawe na fimbo na kuanza kuwashambulia askari na mtuhumiwa wakiwa na lengo la kumuua mtuhumiwa ambapo walimshambulia na kusababisha kifo chake.
Baadhi ya askari wamejeruhiwa, Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Rufaa Bugando kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....