AANGUKIWA NA TAWI LA MTI NA KUFARIKI,NDUGU WAMSUSIA MWILI WA MAREHEMU MTU ALIYEMPA KAZI HIYO....


MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la George Maswizilo (33) amekufa papo hapo baada ya kuangukiwa na tawi la mti. Alikuwa akikata mti huo katika eneo la Mabambasi Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga. Ndugu wa marehemu wamemsusia mwili mtu aliyempa kazi hiyo ili aendelee na maziko.
Tukio hilo lilitokea jana saa mbili asubuhi, ambapo marehemu alikuwa akikata mti katika nyumba ya Magreth Mwandu, aliyempatia kibarua cha kazi hiyo. Baada ya kuukata, mti huo ulimwamgukia na kumbana tumboni, hatua iliyosababisha apoteze maisha akiwa juu ya mti.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema walisikia sauti ya mtu akiomba msaada na walipofika eneo la tukio, walimkuta marehemu akiwa juu ya mti amebanwa na moja ya tawi la mti aliokuwa anaukata. Wakati wakifanya juhudi za kumwokoa, tayari alikuwa ameshapoteza maisha.
Akieleza tukio hilo, Mwandu alisema Maswizilo alifika nyumbani hapo siku moja kabla ya tukio ; na wakaelewana malipo ya Sh 15,000 kwa ajili ya kazi hiyo ya kukata mti na siku iliyofuata, wakati Maswizilo akiendelea na kazi, ndipo mauti yakamfika.
Shangazi wa marehemu aliyejulikana kwa jina la Pili Maswizilo alisema Maswizilo alikuwa anajishughulisha na kazi ndogo ndogo za vibarua kwa kujipatia riziki katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ndembezi David Nkulila alisema tukio hilo ni kama ajali zingine zinazoweza kumpata mtu yeyote na haifai kulaumiana.
“Baada ya kuona inataka kutokea mtafaruku kuhusu tukio hilo, sisi viongozi wa mtaa tulichukua jukumu la kumsaidia mama huyo ambaye ni mjane na hajiwezi, tukafanya mchango kwa wakazi wa mtaa huu na tukafanikisha mpango huo kwa ajili ya mazishi ya marehemu,” Nkulila aliongeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema hakuna mtu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter