MBUNGE wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangala ametaka viongozi wa Chadema waliotoa kauli kuwa wataingilia mchakato wa Katiba wachukuliwe hatua za kisheria na kutishia kuwashughulikia iwapo watakwenda wilayani Nzega mkoani Tabora kuhamasisha wananchi kupinga mchakato huo.
“Ni upuuzi kuwaacha, mtu anasema nchi haitawaliki na wameachwa wanasema wanaingilia mchakato wa Katiba ambao tulikubaliana wote hapa, lakini wakaenda kwa mlango wa nyuma Ikulu kuomba mtu wao apate nafasi na mshauri wa mwenyekiti wao (Freeman Mbowe), Profesa Mwesiga Baregu akateuliwa kuwepo kwenye Tume, sasa wanasema wanaingilia Katiba, wachukuliwe hatua wakiachwa wakaja kwangu Nzega nitahamasisha wananchi huku nikiwaongoza tutawashughulikia,” alisema.
Kigwangala alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Alisema viongozi wa Chadema ni ‘wapuuzi’ kwa kusema Tume ya Mchakato wa kupata Katiba mpya inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba haina weledi wakati ndani yake yupo mwakilishi wao.
“Jifunzeni kuongoza na si kufanya vurugu, mjue Watanzania wameshawaelewa na mkiendelea chama chenu kitakufa kabla ya mwaka 2015,” alisema.
Miongoni mwa wabunge wa Chadema aliyekosoa mchakato wa kupata Katiba hiyo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alisema chama chake kitatembea nchi nzima kuwaambia wananchi kuwa mchakato huo umeingiliwa na viongozi wa CCM hivyo waikatae katiba hiyo mpya.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) alitumia nafasi hiyo kwa kumuita Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) kuwa ni mpumbavu kwa sababu aliwalipa magaidi waliombambikia kesi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare kwa kutumia huduma ya M-Pesa.
Alisema mawaziri wengi wa serikali hawana uelewa hivyo ni wapumbavu, kauli ambayo ilimfanya Spika Anne Makinda amzuie kuendelea kuchangia licha ya kutomaliza muda wake.
Naye Mbunge wa Mkanyageni, Mohammed Habib Mnyaa (CUF) alisema iwapo Bunge au serikali kati ya Aprili na Julai mwaka huu haitamaliza tatizo la gesi kwa kutekeleza matakwa ya watu wa Mtwara kuhusiana na gesi hiyo, atawasilisha bungeni malalamiko katika mkutano ujao wa Bunge.
Alitaja matakwa ya wananchi wa Mtwara kuwa ni kuzalishwe megawati 300 za umeme katika mkoa wao kutokana na gesi hiyo; Lindi na Mtwara ziunganishwe na gridi ya taifa na bandari ya Mtwara iboreshwe ili wakazi wa huko wapate ajira.
Alisema wakazi wa Mtwara hawakatai gesi hiyo kutumika Dar es Salaam.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Longido, Lekule Laizer(CCM) alisema udini uliopo nchini unaundwa na wanasiasa na ni suala ambalo ni balaa, hivyo amewataka wanasiasa hao wasiwafanye wananchi wakawa wakimbizi na kuwataka mashekhe na wachungaji kuhubiri amani
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....