MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula amekiri kuwapo kwa suala la udini chuoni hapo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusiana na malalamiko ya suala hilo, Profesa Kikula alisema hali hiyo inatokana na matakwa ya wanafunzi wenyewe.
“Unakuta wanafunzi wanataka kupangwa kutokana na shule walizotoka au wakati mwingine wengine hutaka kukaa chumba kimoja kwa kuwa tabia hazilingani... wengine ni wanywaji wa pombe, sasa inakuwa ni ngumu kuwaweka watu wenye tabia tofauti. Lakini pia suala hili la udini lilianza miaka mitatu iliyopita kwenye uchaguzi wa serikali ya wanafunzi,” alisema.
Hata hivyo, alisema yeye si mpangaji wa wanafunzi isipokuwa mkuu wa wanafunzi (Dean of Students) ndiye anayewajibika kupanga wanafunzi.
Awali wanafunzi chuoni hapo walimlalamikia Profesa Kikula kwa kupenyeza suala la udini chuoni hapo.
Mmoja wa wawakilishi wa wanafunzi aliyezungumza na Tanzania Daima, alisema hivi sasa hali ni mbaya chuoni hapo, kwani imesababisha mgawanyo kati ya Waislamu na Wakristo.
Mwakilishi huyo alisema hali hiyo inawaathiri kimasomo kutokana na wao kushindwa kujadili baadhi ya masomo kwa pamoja na kusema kuwa imefika mahala wanafunzi wametengewa mabweni ya kulala kutokana na dini zao.
“Wakati mwingine utasikia achana na hao makafikiri, mang’ong’o, kiuhalisia jambo hili ni baya sana, kwani athari zake ni kubwa na chanzo cha yote haya ni Profesa Kikula,” alisema mwanafunzi huyo.
Alieleza kuwa awali chokochoko hizo zilianzia kwenye uchaguzi wa serikali ya wanafunzi mwaka jana ambapo kulikuwa na namna ya kuingiza masuala ya udini na itikadi za vyama.
“Profesa Kikula hayuko pekee yake, kwani anashirikiana na wenzake na alishawahi kuleta masheikh chuoni, jambo ambalo sisi kama wanafunzi wenye imani ya Kikristo tunapatwa na wasiwasi na tunaomba Rais Jakaya Kikwete alishughulikie suala hili,” alisema.
source:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....