MTOTO wa kiume mwenye umri wa siku tatu ametupwa na mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina la Bhoke Masero katika Kijiji cha Nyasaricho, kwa kile kilichodaiwa kuwa ulemavu wa mdomo aliozaliwa nao.
Kwa mujibu wa wazazi wa kijana Chacha Sylvester aliyedaiwa kumpatia ujauzito binti huyo, Scholastica na Sylevester Chacha, mama wa mtoto huyo alimtupa na kumtelekeza mtoto huyo majira ya saa 12.00 jioni nyumbani kwao wiki iliyopita.
Walidai kuwa binti huyo aliyetupa mtoto alifika nyumbani hapo akiwa ameongozana na wazazi wake waliowataja kwa majina ya Kambi Siruri na Paulina Kambi wakiwa na mama mdogo wake ambapo walikiweka kichanga hicho mezani na kutoweka.
Kufuatia tukio hilo, wazazi hao walilazimika kupiga simu kituo cha Polisi Bomani kwani mtoto huyo anapata taabu kunyonya au kunyweshwa chochote kutokana na ulemavu wake wa mdomo. Polisi hao waliwataka kwenda kituoni kuandikisha maelezo.
Walisema walijaribu kuwasihi wazazi hao kutofanya kitendo hicho wakiwa pamoja na Mwenyekiti wa kijiji cha Nyasaricho lakini bila mafanikio.
Mtoto wa kiume mwenye umri wa siku tatu aliyetupwa na mama yake mzazi. |
Ilielezwa kuwa mama mzazi wa mtoto huyo aliamua kuchukua hatua hiyo baada ya mtu aliyedai kumpa ujauzito huo, Sylvester kuukana baada ya kujulishwa.
Gazeti hili lilifanikiwa kufika kwenye tukio, kituo cha Polisi Bomani na Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ambako mtoto huyo aliyelazwa katika wodi namba tano anaendelea vizuri.
Afisa Ustawi wa Jamii wa hospitalini hiyo Abeil Gichaine, alisema mama mzazi wa mtoto huyo anaendelea kutafutwa na polisi pamoja na mambo mengine, aweze kumnyonyesha.
‘’Kwa vile mama mzazi yupo, tunamtafuta ili aweze kumnyonyesha mwanaye,” alisema.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....