Lakini pia bandari hiyo inatafsiriwa kama ‘kiama’ cha bandari kongwe zilizopo jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Kazi hiyo itakayofanywa kwa mkopo wa zaidi ya Shilingi trilioni 16 (Dola bilioni 10 za Marekani), unagharamiwa kwa asilimia 100 na serikali ya China.
Fedha hizo ni sawa na bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.
Wafanyakazi wa bandari hiyo waliokataa kutaja majina yao walipozungumza na NIPASHE Jumamosi, wanaitaka serikali iwaondolee hofu kutokana na taarifa zinazoeleza kuwa mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo, unakataza kuwapo kwa bandari nyingine zinazoshindani nayo.
“Kipengele kimojawapo cha mkataba wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, kinasema kwa umbali wa kilometa 200 za mraba kusini, mashariki, magharibi na kaskazini hakutaruhusiwa kuwapo na bandari ya namna hiyo wala kuendeleza bandari ya namna hiyo,” kinaeleza chanzo chetu.
Chanzo hicho kinasema, “bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara hazitapanuliwa, kuboreshwa wala kuendelezwa ili kutoa nafasi kwa bandari ya Bagamoyo kuwa ya kwanza kwa ubora na bila kuwa na mshindani kwa kipindi cha miaka 50.”
Msemaji huyo anaungwa mkono na mwingine aliyesema, wanaomba serikali iwaeleze ukweli na kuwaondolea hofu, kwa maana hawajajua hatima yao kutokana na mikataba hiyo kufichwa.
UPANUZI GATI namba 14 KUSIMAMISHWA
Wakielezea hofu yao zaidi juu ya mkataba unaokataza upanuzi wa bandari kwenye eneo la kilometa za mraba 200, walisema upanuzi wa gati au (lango) namba 14 katika bandari ya Dar es Salaam umesimamishwa au utasimamishwa mara moja.
Hatua hiyo itachukuliwa ili kuipa ama kuheshimu na kulinda mkataba wa Wachina kwa ajili ya bandari ya Bagamoyo.
WACHINA KUIENDESHA MIAKA 50
Wafanyakazi hao walisema walidokezwa na maofisa wa serikali waliouona mkataba huo kuwa Wachina watapata `ulaji’ unaowaruhusu kufanyakazi ya kuendesha bandari hiyo na kuimiliki kwa miaka 50 baada ya ujenzi kukamilika.
Walisema habari za ndani kutoka vyanzo vya serikalini kuhusu baadhi ya mikataba 16 iliyosainiwa na Rais wa China Xi Jinping, mwezi uliopita wakati alipoizuru Tanzania.
Zilibainisha kuwa ujenzi wa bandari hiyo una masharti magumu ambayo ni pamoja na kufanikisha mradi wa bandari ya Bagamoyo, Tanzania itachukua mkopo wa fedha na vifaa kutoka China.
Mkataba huo vyanzo, viliwaambia wafanyakazi hao kuwa unasisitiza kuwa ujenzi utafanywa na kampuni ya China na wahandisi wake watapewa jukumu la kujenga bandari hiyo pasipo kupitia zabuni.
“Serikali ya China ndiyo itakayoendesha bandari hiyo kwa muda wa miaka 50 kuanzia hapo itakapokamilika ili kurudisha fedha za mkopo zizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo .”
Wafanyakazi hao walisema chanzo kiliwadokeza kuwa, China italazimika kuendesha bandari ili kujirudishia fedha zake za mkopo ilizotoa.
“Lakini inashangaza kwa sababu hakuna kipengele kinachoeleza kuwa endapo watajirudishia mkopo wao na riba kabla ya miaka 50, watarejesha bandari hiyo mikononi mwa serikali,” kilisema na kuongeza kuwa inawezekana fedha hizo zikarudishwa hata kabla ya muda uliowekwa.
Hata hivyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, anajiweka kando na kutoa ufafanuzi za suala hilo, akimuachia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Dk Mwakyembe hakupinga wala kuzikataa hofu za wafanyakazi wa TPA.
ZIARA YA JINPING
Rais wa China Jinping akiwa nchini mwezi uliopita, alisema China imetenga Dola bilioni 20 za marekani kuisaidia Afrika na kwamba itakuwa na ushirikiano wa ulinganifu na wa manufaa kwa pande husika.
Akasema hakutakuwa na masharti magumu kama ambavyo nchi tajirii zimekuwa zikiilazimisha Afrika kuyafuata.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanapingana na hatua ya China na kueleza kuwa hiyo ni janja ya kuiingia Afrika na pale itakapofanikiwa kupenya, itakuwa na ukandamizaji na ubeberu utakaowaumiza Waafrika kuliko ule wa ukoloni mkongwe.
BANDARI YA BAGAMOYO KATIKA MITANDAO
Kwa mujibu wa mikataba 16 iliyosaibiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Jinping wa China, bandari hiyo itagharimu Dola bilioni 10 (sawa na Shilingi trilioni 16).
Taarifa hii imo kwenye tovuti za Tanzania, About Tanzania, Tanzania Investment Economic and Business News Interviews Reports Consulting na Military News Humor Photos - StrategyPage
Mitandao inawakariri maofisa wa Tanzania wakisema, China itawekeza zaidi ya Dola milioni 800 kujenga miundo mbinu itakayousukuma mbele uchumi wa taifa hili.
Kwa upande wa bandari ya bandari ya Bagamoyo inatarajiwa kukamilika 2017.
Chini ya makubaliano hayo ya Tan-cino (Tanzania na China) kutakuwa na mikataba mingine ya kukopa itakayofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Benki ya China ya kuuza ng’ambo na kuagiza bidhaa nje.
Pia kuna mikataba ya kuanzisha viwanda vya kisasa, kanda za kiuchumi za kilimo na kufunguliwa kituo cha utamaduni na mila za watu wa China.
Makala haya yameandikwa na Gaudensia Mngumi, kwa msaada wa mtandao.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....