Marehemu Martha Charles baada ya kuchinjwa shingoni na mume wake.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Afande Onesmo Lyanga alisema tukio hilo lilitokea katikati ya wiki iliyopita ambapo pia alimtaja mume anayedaiwa kutekeleza unyama huo kuwa ni Asack Nzolela (29), mfanyabiashara wa bucha la nyama ya ng’ombe.
Afande Lyanga alisema mtuhumiwa alimchinja mkewe wakiwa wamelala chumbani kwenye nyumba ya wazazi wa mwanaume huyo na baada ya kufanya ukatili huo alikimbia.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka katika familia ya marehemu zilisema chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia ambapo mtuhumiwa alianza kwa kumlaumu mama yake mzazi kwa kitendo cha kumtafutia kazi mkewe katika Halmashauri ya Mji wa Kahama wakati yeye alikuwa hataki mkewe afanye kazi.
Habari zilizopatikana eneo la tukio kutoka kwa mmoja wa ndugu anayeishi na familia hiyo, Paul Edward alisema mbali na kuchinjwa shingoni pia marehemu alikatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Edward alisema usiku wa tukio akiwa amelala katika moja ya chumba ndani ya nyumba hiyo, alisikia kelele za ugomvi kutoka kwenye chumba cha wanandoa hao hali iliyomfanya apige kelele zilizowafikia majirani ambao walifika kutoa msaada.
Akasema majirani hao sanjari na yeye walimkuta mtuhumiwa ameshamchinja mkewe kwa kisu na kutoweka kusikojulikana.
Nao majirani waliokwenda kutoa msaada ambao hawakupenda majina yao yatajwe gazetini, walisema walikuta mwili wa Martha ukiwa kitandani huku amekatwa na kitu chenye ncha kali katika eneo lote la shingo, ndipo walipomchukua na kumkimbiza hospitali lakini tayari alikuwa ameshakata roho.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Noel Mkisi alisema baada ya muuaji huyo kutoroka usiku huohuo jitihada za kumsaka zilianza.
Tukio la kuchinjwa kinyama kwa mwanamke huyo limetokea siku chache baada ya hivi karibuni, mchuna ng’ombe Musa Petro (27) naye kumuua kwa kumchinja kwa kisu mpenzi wake, Jessica Elialinga (19).
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Maduka ya Nyama Kahama, Faraji Mohamed akiongea na mwandishi wetu alisema Petro ni mfanyakazi wa Nzolela katika duka lake la nyama (bucha) ambapo alishangaa kusikia Nzolela amemchinja mke wake kama alivyofanya mfanyakazi wake, Petro.
Wakati tunakwenda mitamboni habari zilizopatikana kutoka Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kahama na kudhibitishwa na OCD George Simba zilisema mtuhumiwa huyo amekamatwa.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....