MWANAMKE mmoja ambaye ni mke wa mtu aliyejulikana kwa jina la Atupele mkazi wa Mtaa wa Masewe Kata ya Ilemi, jijini hapa, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya wakazi wa eo hilo kumpa kibano wakimtuhumu kwa ushirikina.
Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni baada ya mtoto aliyetambuliwa kwa jina la Judith Chengula (3) kupotea katika mazingira ya kutatanisha, Februari 22, mwaka huu.
Kwa mujibu wa wakazi hao, mtoto huyo alipotea majira ya saa 11 jioni wakati alipokuwa akitoka kanisani na dada yake aitwaye Anitha Mgaya.
Imeelezwa kwamba, baada ya wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kumtafuta Judith bila mafanikio, walikaa vikao kadhaa lakini Atupele hakuhudhuria.
Habari zinadai kwamba, kitendo cha mtuhumiwa huyo kutohudhuria kwenye vikao hivyo kiliwapa mashaka na kuhisi huenda mama huyo anahusika na kupotea kwa Judith.
Imedaiwa kwamba Machi 23, mwaka huu asubuhi wananchi hao waliendelea kusisitiza Atupele achukuliwe hatua lakini baadaye waliamua kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alidai kuwa, baada ya kufanya upekuzi nyumbani kwa mama huyo walikuta vitu vilivyodaiwa ni vitovu vya watoto wachanga, hivyo kuamsha hasira kwa raia.
“Mama huyo alipobanwa alijikuta akibabaika ndipo watu wakamvaa kabla ya kuokolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa huo, Nedy Mwamlima aliyempeleka polisi kwa usalama wake.
“Kwa hasira, wananchi wa aneo hilo waliingia ndani ya nyumba ya mama huyo na kutoa nje vitu mbalimbali kisha kuvichoma moto, pia walibomoa nyumba yake na kuharibu mazao yaliyokuwa nje ya nyumba hiyo,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo, gazeti hili linalaani watu kujichukulia sheria mkononi na kwamba, yanapotokea mazingira kama hayo ni vyema vyombo vya dola vikataarifiwa ili viweze kuchukua hatua sahihi badala ya kile walichokifanya wananchi wa eneo hilo-Mhariri.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....