SABABU za aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Cord, Raila Odinga kushindwa katika uchaguzi uliofanyika Machi 4, mwaka huu nchini Kenya na Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi, zimebainika.
Wachambuzi mbalimbali wa siasa za Kenya wamesema sababu kubwa ni Odinga kukosana na washirika wake wengi ambao walimuwezesha kufanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka 2007, akiwemo William Ruto ambaye harakati zake zilimfanya ashitakiwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC japokuwa hakuwa mgombea urais.
Imeelezwa kwamba kujitoa kwa Ruto ni pigo kubwa kwa Odinga kwani ni mmoja wa wanasiasa wenye uwezo mkubwa wa kuzungumza na kushawishi wapiga kura. Eneo analotoka Ruto la Bonde la Ufa ambalo mwaka 2007 lilitoa kura nyingi kwa Odinga safari hii, hawakumpa.
Aidha, baadhi ya watu wamesema Odinga amekosa kura kutokana na kupewa uwaziri mkuu na watu kuona kwamba hakufanya chochote kwa maendeleo yao na kwamba walitarajia angefanya makubwa bila kujua kwamba alikuwa chini ya Rais Mwai Kibaki aliyekuwa akiongoza serikali.
Sababu nyingine inayotajwa ni Odinga kuungana na Kalonzo Musokya ambaye baadhi ya wananchi wa Kenya wanaamini kwamba alifanya makosa makubwa ya kuunga mkono matokeo ya kura za mwaka 2007 yaliyompa ushindi Kibaki na wananchi hao kuona kwamba alifanya vile kwa sababu ya kutaka cheo serikalini ambacho alikipata.
Kalonzo alikuwa Makamu wa rais katika serikali ya Kibaki.
Tayari Kenyatta anayetarajia kuapishwa Machi 26, mwaka huu amesema atashirikiana na wapinzani wao wa Cord chini ya Odinga kuijenga nchi yao.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....