Continued after the jump ....
Si jambo la ajabu kumuona rapa Curtis James Jackson III ‘50 Cent’ akipanda ndege pale New York City, Marekani hadi Sudan Kusini barani Afrika kwa ajili ya kugawa chakula cha msaada kwenye jamii inayokufa kwa njaa. William Leonard Roberts II ‘Rick Ross The Boss’, si mjinga anapoamua kuingia gharama na kwenda kule Lagos, Nigeria kwa walalahoi kisha kushiriki nao katika maisha ya kilofa. Hawa wote wanajua malipo yao. Si fedha.
Huku kwetu ulimwengu wa tatu, wiki iliyopita kulikuwa na vilio pale kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Alirejeshwa nyumbani mwigizaji mchekeshaji, Tumaini Mwakibibi ‘Matumaini’ akiwa hoi akitokea Maputo, Msumbiji alikougua hadi akafikia steji ya kuombewa msaada ili arejeshwe nchini kwa matibabu.
Baada ya Matumaini kufikishwa kwenye ardhi ya nyumbani ndipo akapelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ilala ya Amana, Dar kwa matibabu.
Habari zilidai kuwa alikuwa akisumbuliwa na shinikizo
la damu la kupanda (high
blood pressure), homa kali
na miguu kuwaka moto.
Kweli alipatiwa matibabu na kurejeshwa nyumbani akiwa bado hajapona kabisa.
Namzawadia sentensi moja ya pole kwa yote yaliyompata. Ni mitihani ya maisha na lazima yaendelee. Pole Matumaini!
Hapa ndipo kuna ujumbe kwenu ninyi wasanii mliozoea kuendekeza tambo, maringo, dharau na majivuno kwa jamii bila kujali kuwa kuna kujitoa ili na wewe ukifikwa, jamii ijitoe kwako.
Kabla ya kurejeshwa nyumbani, kulikuwa na taarifa kuwa unahitajika msaada wa hali na mali hasa fedha kwa ajili ya kumsafirisha kwa ndege hadi Dar kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Chama cha Waigizaji Bongo walijitolea na kwenda kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuomba msaada kwa mtu yeyote aliyeguswa na tatizo la staa huyo. Hivi mnajua kilipatikana kiasi gani cha fedha? Madai ni kwamba ilipatikana noti moja ya elfu kumi kutoka kwa msanii mmoja mkubwa wa filamu za Kibongo ambaye hakutaka jina lake litajwe popote.
Si wasanii wala jamii iliyoguswa na tatizo la mchekeshaji huyo. Ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla aliyefuta aibu hiyo kwa kutuma tiketi ya ndege iliyomsafirisha hadi Dar. Saluti kwake!
Kuna mtu anabisha kuwa hapo kuna somo kwa msanii mmoja mmoja au makundi na vyama vyao? Ninyi kama wasanii mmejiuliza tatizo liko wapi? Mnataka niwakumbushe machungu kuwa hata kwa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ilikuwa ikihitaji Sh. milioni 18 akatibiwe India lakini alilazimika kufanya shoo kutafuta fedha hiyo hadi alipodondoka jukwaani?
Ipo mifano mingi, yupo mchekeshaji Said Ngamba ‘Mzee Small’ hana msaada kwa ajili ya matibabu. Yupo Maalim Gurumo, Ramadhani Mrisho Ditopile ‘Mashaka’ na wengine wanaohitaji kusaidiwa kwa matibabu. Kwa nini watu hawajitoi?
Kama wasanii mtakuwa hamjapata somo kupitia mifano hii, basi subirini zamu yenu ikifika. Nawapongeza wale wote wanaojitahidi kujitoa kwa ajili ya jamii. Niliwahi kuandika hapa kuwa kuna njia nyingi za kurudisha kwa jamii ili kutengeneza ‘CV’ ya kupendwa na kupata sapoti unapokuwa kwenye janga. For the love of game!
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....