Rais Jakaya Kikwete ameanzisha mawasiliano na viongozi wa vyama vya siasa vyenye hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa karibuni na Bunge kwa nia ya kuandaa mkutano kati yake na viongozi wa vyama hivyo.
Taarifa Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema kuwa mawasiliano hayo yalianza jana, kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.
”Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu inaangalia uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 ama Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu,” ilisema sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.
Taarifa hiyo pia alisema kufuatia matukio yaliyotokea Bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa Muswada huo mwezi uliopita, na maneno na kauli mbali mbali ambazo zimetolewa na wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wengine kufuatia kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi Ijumaa iliyopita alisema hoja na kauli za wanaopinga Muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya.
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia na kutoka nje wakati wa kujadili na kupitishwa kwa mudwada huo wakidai kuwa ulikuwa na kasoro kadhaa.
Kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha Rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni.
Vyama hivyo licha ya wabunge wake kususia Bunge, pia vimeunda ushirikiano wa kupinga mchakato wa katiba kwa maelezo kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tayari wenyeviti wake Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi) wameshafanya mikutano ya kadhara jijiji Dar es Salaam na Zanzibar na kesho kutwa vyama vyao vimeandaa maadamano ya nchi nzima na baadaye kufanya mikutano mingine katika mikoa yote kuwashawishi wananchi waukatae mchakato huo.
Aidha, vyama hivyo na makundi ya wanaharakati wanamtaka Rais Kikwete asiusaini muswada huo kwa maelezo kuwa utaleta katiba mbovu ambayo haina malahi kwa taifa.
Katika hatua nyingine, Ikulu imekanusha taarifa ambazo jana ziliingizwa katika mitandao ya kijamii na kusambazwa zikidai kuwa Rais Kikwete ametia saini muswada huo.
Ikulu ilisema Kwanza, Ofisi ya Rais haijapokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba inawezekana muswada huo umekwishakutumwa kutoka Bungeni, lakini haujamfikia Rais, hivyo, kama haujamfikia, hawezi akawa ameutia saini
Iliongeza kuwa muswada huo ukimfikia Rais, inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu umepitia katika mchakato sahihi na halali wa kikatiba kwa maana ya kufikishwa Bungeni na Serikali, kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.
Kwamba kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa katika Sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Rais kuwa ametimiza matakwa ya kikatiba ya kutia saini muswada ambao umepitishwa na Bunge kwa kufuatia mchakato sahihi na halali wa kikatiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Sheria kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Rais na baadaye kufanyiwa marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya marekebisho hayo na kutoa mfano kwamba mwishoni mwa mwaka 2012, Sheria ya Marekebisho ya Katiba ilipitia njia hiyo.
MBOWE AMTETEA LISSU
Wakati huo huo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amekumbusha kwamba hotuba yoyote inayowasilishwa bungeni na Waziri Kivuli ni ya kambi hiyo na siyo hoja ya mbunge anayeisoma.
Mbowe aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa siku nne wa wataalam mbalimbali wa Chadema kutoka kanda za kichama.
Alisema haikuwa sahihi kwa Rais Kikwete kumshambulia Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, wakati wa hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa sababu alisoma kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Lissu pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa kambi hiyo.
“Lissu alitimiza wajibu wake wa kikanuni ndani ya Bunge kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa hiyo kitendo cha Rais kumshambulia na kulitangazia Taifa uhasama na Lissu hakumtendea haki na kwa mtu muungwana anapaswa kumwomba radhi Lissu,” alisema.
Alisisitiza kwamba taarifa ya Lissu kuhusu kutoshirikishwa Zanzibar kwenye mchakato wa maoni kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na ile ya uteuzi wa wajumbe, haina uongo wowote.
Mbowe alisema hata baada ya wabunge wa upinzani kuomba mwongozo na kunyimwa fursa hiyo hadi wakaamua kutoka nje, wabunge wa CCM waliobaki ndani hawakujadili muswada badala yake walirusha vijembe na kejeli kwa kambi ya upinzani.
“Kwa hiyo Rais anaposema mjadala wa Bunge ulikwenda vizuri ajue kwamba amepotoshwa kwa makusudi. Watu waliomweleza rais taarifa hizi ni akina Lukuvu (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) na Wasira (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu), ambao walikuwa wanaturushia vijembe bungeni, Rais asome hansadi aone kilichojadiliwa,” alisema.
Alisema mchakato wa Katiba siyo jambo jepesi kama baadhi ya viongozi wa CCM wanavyodhani kwa kuwa ni suala ambalo linaweza kuipasua nchi.
Akilihutubia Taifa Ijumaa iliyopita, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, alisema kauli ya Lissu ni uongo, uzushi, unafiki, hiana na uzandiki kwa kusema Zanzibar haikushirikishwa wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliwasilisha maoni yake na kwamba uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Katiba ulizingatia mapendekezo ya wadau wote.
Kuhusu kauli ya Rais ya kuwataka viongozi wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kusitisha maadamano ya Alhamisi kupinga mchakato wa katiba badala yake kuwaita kwenye mazungumzo, Mbowe alisema hayo yatazungumzwa katika mkutano wa pamoja wa vyama hivyo.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, jana ilianza vikao vyake, huku muswada huo ukiwa haumo kwenye ratiba ya shughuli za vikao vya kamati hiyo.
Kutokana na hali hiyo Lissu alisema hatua hiyo inamaanisha kwamba kauli ya Rais Kikwete kwamba, baadhi ya mambo yanayolalamikiwa na wapinzani kwenye muswada huo yanazungumzika, siyo ya kweli.
Ratiba ya shughuli za Kamati hiyo ilitangazwa jana na Makamu wake, William Ngeleja, katika mahojiano na waandishi habari muda mfupi baada ya kuahirisha kikao cha kamati yake, jijini Dar es Salaam.
Ngeleja alisema kikao cha jana ambacho alisema ni katika vikao vya kawaida vya kamati yake, kilifanya kazi moja ya kupitia ratiba ya shughuli, ambazo watazifanyia kazi.
Alisema katika ratiba hiyo, watajadili miswada miwili pekee; wa Kura ya Maoni na wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.
Lissu alisema kitendo cha muswada huo kutopelekwa kwenye kamati kinamaanisha kwamba haurudi bungeni.
Alisema hali hiyo ni kinyume cha kauli ya Rais Kikwete kwamba, muswada huo unazungumzika bungeni.
“Namna ya kuurudisha bungeni ni lazima upitie kwenye kamati. Sasa utarudi lini bungeni? Anajua Rais,” alisema Lissu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....