SIMBA WATISHIA KUGOMEA MECHI NA YANGA BAADA YA REFA KUBADILISHWA GHAFLA...!!

UONGOZI wa Simba SC umesema hauna imani na mabadiliko ya refa yaliyofanywa kuelekea mpambano wao na Yanga SC Jumamosi na kwa sababu hiyo unakutana katika kikao cha dharula haraka iwezekanavyo kujadili suala hilo, ikibidi kususia mchezo huo.

Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba inayosimamia ushiriki wa timu katika mashindano pia, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba uongozi utakutana haraka kujadili mabadiliko hayo.

Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema taarifa rasmi waliyokuwa nayo awali refa aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo ni Israel Nkongo, lakini ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo limemtaja refa tofauti, Martin Saanya.

“Haiwezekani mabadiliko yafanyike ghafla, lazima kutakuwa kuna namna hapa. Tunakutana mara moja kujadili na kuchukua hatua, ikiwezekana tunaweza kugomea hiyo mechi, iwapo tutagundua kuna mchezo mchafu umeandaliwa dhidi yetu,”alisema Hans Poppe.

Saanya kutoka Morogoro ndiye ameteuliwa kuchezesha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga SC la kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka nchini ili kujionea nani zaidi baina ya miamba hiyo, Saanya atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, wakati refa akiba atakuwa ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.

Kamisaa wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi atakuwa ni Leslie Liunda wa Dar es Salaam.

Mashabiki watakaotaka kwenda kushuhudia mpambano huo wa mahasimu wa jadi katika soka ya Tanzania, watalazimika kulipa Sh. 5,000, hicho kikiwa kiingilio cha chini zaidi katika sehemu ya viti vya Rangi ya Bluu.
Aidha, katika mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, viingilio vingine ‘nafuu kidogo’ vitakuwa ni Sh 7,000 kwa viti ya Rangi ya Kijani na Sh. 10,000 kwa viti vya Rangi ya Chungwa.

Upande wa ‘wakubwa’, viingilio vitakuwa ni Sh. 15,000 kwa VIP C, Sh. 20,000 kwa VIP B na Sh. 30,000 kwa VIP A.

Ofisa Haabri wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kwamba viingilio hivyo ni sawa na viingilio vya mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo baina ya miamba hao, Oktoba 3, mwaka jana.
Wambura alisema tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo, yaani Ijumaa wiki hii katika vituo mbalimbali vitakavyotajwa.

Tayari miamba hiyo ya soka nchini iko mafichoni kwa maandalizi ya mpambano huo.
Yanga wameweka kambi yao kisiwani Pemba katika hoteli ya Samail mkabala na benki ya PBZ, wakifanya mazoezi Uwanja wa Gombani wakati Simba wameweka kambi maeneo ya Mbweni, Zanzibar wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung.

Wakati Yanga walitua Pemba Ijumaa jioni, mahasimu wao wa jadi, Simba SC waliwasili Zanzibar Jumapili jioni na mara moja kuanza kujifua kwa ajili mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter