Kutokana na hali hiyo, waumini hao wanadaiwa kuweka msimamo wao kwamba endapo kiongozi huyo hataondolewa, wapo tayari kulihama kanisa hilo
KWA NINI KANISA LITIKISIKE?
Siku za karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya baadhi ya viongozi wa kanisa hilo kudaiwa kushiriki vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni vya uzinzi.
Hivi karibuni Padri Urbanus Ngowi wa Jimbo la Moshi alidaiwa kufumaniwa na mke wa mtu aliyejulikana kwa jina moja la kijamii la Mama P.
Mbali na Padri Ngowi kunaswa na mwanamke huyo na picha zake kutolewa kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda Toleo la 313 la Aprili –Mei 5, 2013, pia Padri Celestine John Nyaumba wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Homboro Dodoma anadaiwa kumjeruhi mwanamke aliyezaa naye, Selestina Anania Kibena licha ya kwamba sheria za kanisa hilo haziruhusu mapadri kuzaa wala kuoa.
TURUDI KWA MCHANUZI
Mchanuzi, licha ya kudaiwa kuwa na nyumba ndogo pia waumini hao wamedai amekwenda mbele zaidi kwa kuamua kumjengea mwanamke huyo nyumba ya ghorofa Tabata Kinyerezi, Dar.
PAROKO AINGILIA KATI
Madai hayo yalivuma kiasi kwamba, paroko wa parokia hiyo, Cyprian Kagaba (pichani) aliamua kuingilia kati kwa kuitisha vikao kwa nyakati tofauti na wajumbe wa Kigango cha Kimanga na Jumuiya Kuu ya Mtakatifu Martin ili kujua nini tatizo au kiini cha kuwepo kwa madai hayo mazito.
WAUMINI WAMUITA KADINALI PENGO
Licha ya kutopatikana kwa suluhu kupitia vikao vilivyoitishwa na Paroko Kagaba, baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamemuomba Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Tanzania, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo kufika kanisani hapo ili kuweka mambo sawa.
Waumini hao wamedai kwamba pamoja na paroko wa kanisa hilo kuingilia kati kwa kuitisha vikao lakini bado hali si shwari wakisisitiza mwenyekiti huyo ang’oke.
“Suala hili la mwenyekiti limeleta mgawanyiko mkubwa ndani ya kanisa hali inayohatarisha usalama na kurudisha nyuma maendeleo ya kanisa,” alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo huku akiomba jina lake lisiandikwe gazetini.
WASIWASI FEDHA ZA KANISA KUJENGA GHOROFA Waumini hao waliendelea kudai kwamba wana wasiwasi kwamba fedha alizotumia mwenyekiti huyo kumjengea ghorofa mwanamke huyo, zinaweza kuwa za kanisa kwa vile hakuna taarifa yoyote inayotolewa kwa waumini au wajumbe wa kanisa hilo kuhusu matumizi ya fedha.
Ilibainika kuwa chanzo cha kuzuka kwa madai hayo ya kuwepo kwa nyumba ndogo ni matumizi hayo ya fedha ambapo mwenyekiti huyo anasimamia.
Waumini hao waliendelea kudai kuwa matumizi mabaya ya fedha yalisababisha baadhi ya viongozi kujiuzulu akiwemo aliyekuwa katibu, Perpetua Mashele ambaye alimwandikia barua Paroko Kagaba juu ya dhumuni la kuachia ngazi.
Barua hiyo (nakala tunayo) iliandikwa Aprili 10, mwaka huu ikieleza kwamba shughuli aliyokuwa akipaswa kuifanya kikatiba ameporwa na kufanywa na viongozi wachache kwa manufaa yao binafsi.
Katika barua hiyo, aliyekuwa mweka hazina ambaye pia alijiuzulu, katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitatu hakuwahi kwenda benki kushughulikia fedha za kanisa hilo zaidi ya mwenyekiti huyo.
UWAZI LAMSAKA MWENYEKITI
Baada ya kusikia madai hayo yote wiki iliyopita, Uwazi lilimtafuta Mchanuzi ili kusikia kutoka kwake kuhusu madai hayo ambapo kwa upande wake alikiri kuwepo kwa manenomaneno hayo.
Alisema wapo watu wachache wanaovumisha kwamba ana nyumba ndogo na taarifa hizo wamezieneza kila sehemu hadi kwa paroko wa parokia hiyo, akimaanisha Cyprian Kagaba.
Aliendelea kusema kwamba mwanamke anayedaiwa ni nyumba ndogo yake alikuwa mke wake wa pili wa ndoa tangu mwaka 1993 lakini waliachana mwaka 2003 yeye alipojiunga na kanisa hilo.
Alisema kwa sasa amebaki na mke mmoja wa ndoa aliyemuoa mwaka 1970, hivyo aliyemuacha si mke wake tena.
KUHUSU MADAI YA KWENDA KWA NYUMBA NDOGO KILA MARA
Mwenyekiti huyo aliweka wazi kwamba ni kweli amekuwa akienda nyumbani kwa mwanamke huyo kwa sababu ya kuwaona watoto watatu aliozaa naye na si kukutana naye kimwili.
“Watu hao wanaonipiga vita wamewahi kunitegea hadi mwanamke ili nifumaniwe naye gesti lakini hawakufanikiwa. Hili suala la nyumba ndogo limeshafika hadi kwa Pengo wala si suala geni kwangu,” alisema mwenyekiti huyo.
VIPI KUHUSU KUMJENGEA GHOROFA?
“Si kumjengea, bali nilimuongezea kiasi cha fedha alizolipwa kama fidia na serikali wakati anahamishwa pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ili kupisha upanuzi wa uwanja huo na nilifanya hivyo kwa sababu ana watoto wangu, ubaya uko wapi jamani? Mimi nilimuongeza fedha kidogo lakini nyingine zilikuwa za kwake.”
Kuhusu matumizi mabaya ya fedha, mwenyekiti huyo alisema si ya kweli kwa vile kila kitu kinajulikana kwa paroko na watu wengine wanaostahili kujua.
PAROKO KAGABA HUYU HAPA
Kwa upande wake, Paroko Kagaba alikiri kuwepo kwa uvumi kuwa mwenyekiti huyo ana nyumba ndogo. Akasema alishafanya uchunguzi na kugundua kuwa ni yule mwanamke aliyeachana naye wakati anajiunga na kanisa hilo.
Aliendelea kusema kwamba kwa upande wa fedha zipo salama na amekuwa akiwaita wajumbe wenye madai hayo na kuongea nao ili wawe kitu kimoja na waondokane na uvumi.
“Hivi karibuni tulikutana mapadri wanne wa kanisa hili la Tabata kujadili mambo hayo yaliyokuwa yakikua kwa kasi, niliwaambia lazima waumini waachane na uvumi,” alisema paroko huyo.
AONAVYO MHARIRI
Kwa mujibu wa imani ya Kikristo, mwanaume anatakiwa kuoa mke mmoja tu, hivyo Mchanuzi ili awe muumini safi wa kanisa hilo aliamua kufuata sheria za imani hiyo kwa nia njema kabisa kwa kumuacha mke wa pili licha ya kuzaa naye watoto watatu. Ni maamuzi magumu lakini sahihi.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....