BAADA YA KUFANYA UFISADI WAZIRI NTAGAZWA ADAIWA KUJIFICHA CHOONI AKIKWEPA KUKAMATWA NA POLISI....!!


SAJENTI Albogasti Kashaija (40), ameieleza Mahakama kuwa Waziri wa zamani, Arcado Ntagazwa, anayekabiliwa na mashitaka ya kujipatia mali za Sh milioni 74.9 kwa njia ya udanganyifu alijificha bafuni ili asikamatwe na askari.

Aidha alidai kuwa mshitakiwa huyo aliwahi kutoroka chini ya ulinzi wa Polisi, lakini walifanikiwa kumkamata nyumbani kwake baada ya kugoma kutoka ndani kwa saa nne.
Shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashitaka, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Gane Dudu, wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Charles Anindo, alidai kuwa baada ya Ntagazwa kutoroka kituo cha Polisi, ambapo alishikiliwa baada ya kushindwa kutimiza ahadi ya kulipa deni la Sh milioni 74.9, walikwenda nyumbani kwake Mbezi kumkamata.
Alidai walipofika nyumbani kwa mshitakiwa saa 12 asubuhi na kugonga mlango katika utaratibu wa kawaida, hakufungua, walipomuagiza kijana wake wa kazi, hakutoka pia licha ya kuambiwa kuwa wao ni askari.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kukaa kwa muda mrefu, walimuita Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mbezi na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, ambaye alimpigia simu ili atoke, lakini aliwajibu kuwa bado anasoma magazeti ndipo waliingia chumbani kwake na kumkuta kavaa pensi akakimbilia bafuni.
Aidha shahidi huyo alidai kuwa mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo Senetor Julius, alimueleza kuwa Ntagazwa ndiye aliyemtuma akachukuwe fulana 5,000 na kofia 5,000 kwa Noel Severe.
Katika maelezo yake aliyoyatoa kituo cha Polisi, Julius alidai kuwa walikuwa wanatarajia kutengeneza fulana hizo kwa kutegemea wafadhili kutoka Uholanzi, lakini mfadhili huyo alikatisha mkataba wake baada ya kupata taarifa kuwa zilikuwa za chama cha CCJ.
Katika mkataba wao, inadaiwa washitakiwa, walidai wanachapisha nguo hizo kwa ajili ya sare za kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mbali na Ntagazwa washtakiwa wengine ni Senetor Mirelya (60) na Webhale Ntagazwa.
Wanadaiwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani Mikoroshini, kwa nia ya kutenda ovu walijipatia fulana 5,000 na kofia 5,000 zenye thamani ya Sh milioni 74.9 kutoka kwa Severe kwa makubaliano kuwa wangemlipa fedha hizo katika kipindi cha mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa kumlipa.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter