"KOMENI KUJADILI MWENENDO WA KESI YA LWAKATARE NJE YA MAHAKAMA"....HAPPINESS KITABAZI

BAADHI ya wabunge, wanahabari na wananchi wengine wote wanaoijadili  kesi ya jinai PI,6/2013 ya Jamhuri Vs Wilfred Lwakatare na Ludovick iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Alocye Katemana wameamua kwa makusudi kuingiza uhayawani wao kwa  kuijadili kesi hii nje ya mahakama wakati tayari mawakili wa serikali walishasema Machi 22 mwaka huu, siku kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa kuwa upelelezi bado haujakamilika na kesi hiyo ikaarishwa hadi Aprili 17 mwaka huu, kwa ajili ya kuja kutajwa.

Si mahakama, bunge wala Wizara ya Habari inapiga marufuku vyombo vya habari kuchapisha au kutangaza maoni ya watu wanayoyatoa kuhusu kesi hiyo ambapo maoni mengi yanajithibitisha wazi kuwa watu wanaijadili kesi hiyo nje ya mahakama.

Hao hao wanaoijadili kesi hiyo ya Lwakatare nje ya mahakama na wengine kujifanya wanamuonea huruma sana Lwakatare ni wanafki! Hatujawaona wala kuwasikia hata siku moja wakibeba hata dumu moja la maji wakampelekea Lwakatare katika gereza la Segerea.

Wengi wanaojifanya leo hii wanaisemea hiyo kesi ya Lwakatare ukiwauliza walishatoa hata mchango wa nauli kwa mke wake Lwakatare wa kumuwezesha kila siku kumpelekea mume chakula Gerezani, hawajawahi kufanya hivyo.

Wanajitafutia umaarufu kwa kuijadili kesi ya Lwakatare ambapo kwa ujinga wao huo hawajui kuwa wataendelea kumkandamiza Lwakatare bila sababu za msingi.

Tuwaulize hawa wabunge wanaojifanya wanaijadili sana hii kesi nje ya mahakama, wao si wabunge wa wananchi? Mbona huko majimboni mwao kuna wananchi wao, tena waliowapigia kura, nao wamefunguliwa kesi za zinazotaka kufanana kama za mauji, utakatishaji fedha haramu n.k., ambazo nazo ni kama kesi ya ugaidi inayomkabili Lwakatare ambazo hazina dhamana, mbona wabunge hawa hawapayuki kama hivi kuwatetea wananchi hao na kusema kuwa wamebambikiwa kesi?

Kwa nini baadhi ya waandishi wahabari, baadhi ya wanasiasa uchwara ambao ni maamuma wa sheria  kutwa kuijadili 
kesi ya Lwakatare nje ya mahakama kuwa kesi hiyo ni ya kubambikiwa?

Mbona tumemshuhudia aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, Daniel Yona, Rajabu Maranda, David Mattaka, Idd Simba na watu wengine wenye nyadhifa kubwa walipofunguliwa kesi pale Mahakama ya Kisutu, wanasiasa nyie hamkujitokeza kupayuka hadharani kuwa nao wamebambikiwa kesi?

Ninachokumbuka, ni hawa hawa wanasiasa wa upinzani ambao kipindi hicho cha mwaka 2008 walikuwa wakishinikiza serikali iwafikishe mahakamani vigogo wa CCM ambao wanatuhumiwa kwa ufisadi. Kweli baadhi ya vigogo waliokuwa wakituhumiwa walifikishwa na wengine walipatikana na hatia wakafungwa, mfano ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba na Kada wa CCM, Rajabu Maranda wakati aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin walishinda kesi yao uhujumu uchumi.

Baadhi ya wanasiasa na wanahabari walianza kusema kesi hizo ni danganya toto na hakuna atakayekutwa na hatia lakini mwisho wa siku baadhi ya washitakiwa walikutwa na hatia.

Hiyo ndiyo aina ya wananchi wa nchi yetu wa Tanzania. Wengi wetu tumejenga kasumba ya kudandia gari kwa mbele yaani ‘kujadili hoja fulani bila kujua undani na uhalisia wake’.

Pili, tunapenda sana kushinikiza hatua fulani zichukuliwe dhidi ya watu fulani bila hata ya kufahamu kuwa suala la kumfikisha mtu mahakamani linahusisha wanataaluma ambao ni wapelelezi na wanasheria. Hawa ndiyo tumewapa jukumu la kupeleleza na kuwafungulia kesi watuhumiwa mahakamani pindi wanapoona kuna ushahidi wa kuweza kuwafungulia kesi.

Lakini mbaya zaidi vyombo hivyo vinapoanza kufanyakazi kwa watu ambao sisi tunamapenzi na maslahi binafsi na washitakiwa ambao wamefunguliwa kesi  mahakamani, basi ni sisi tunageuka na kuanza kuvishutumu vyombo hivyo kuwa vinaonea watu na kuwabambikizia kesi watu.

Sisi wasomi wa sheria tunasema kwamba jukumu la kusema mshitakiwa ametenda kosa au hajatenda kosa ni la mahakama na siyo la wanasiasa ‘uchwara ’ ambao wanataka kuparamia majukumu ya mahakama ya kutoa haki na kutafsiri sheria wakati jukumu la mhimili wa bunge na wabunge ni kutunga sheria!

Ni wabunge hawa hawa ambao leo hii wanaijadili kesi ya Lwakatare iliyopo mahakamani, ndiyo Bunge lao limetunga sheria hiyo ya ugaidi, lakini leo hii  sheria hiyo imetumika kumshitaki Kaka yangu Lwakatare, ambaye ni mwanasiasa mwenzao, wanaiona mbaya. Tuwahoji siyo wao ndiyo waliyoipitisha sheria hii?

Hivi si ni hawa wabunge  ndiyo kutwa tunawasikia wakilalamika kuwa mhimili wa serikali unauburuza mhimili wa Bunge na kwamba hawapendi tabia hiyo?

Sisi wadau wa mahakama tunatoa rai kwa mhimili wa mahakama utoe amri ya kuitaka jamii, wabunge, vyombo vya habari n.k., kuacha mara moja kuijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama. Hili linawezekana kwani ninakumbuka mwaka 2007 Jaji Salum Massati wakati akiwa jaji wa Mahakama Kuu, alitoa amri ya kuzuia mtu yeyote kulijadili suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi hadi shauri lilokuwa mbele yake -- ambalo lilifunguliwa mahakamani hapo na Mchungaji Christopher Mtikila -- atakapolitolea uamuzi.

Madhara ya kuacha jambo hili lijadiliwe nje ya mahakama ni wazi linapandikiza chuki baina ya ndugu na familia ya Lwakatare na serikali kwa maana Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi ndiyo aliyeifungua kesi hii kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 90 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Wanahabari mnaoijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama, achei unafiki wa kutumika vibaya na upande mmoja wa vyama vya siasa. Kwani ninyi wanahabari mpo karibu sana na Lwakatare kuliko wanahabari wenzenu ambao ni  Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda na Samson Mwigamba na Theophil Makunga  ambao nao wanakabiliwa na kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi katika gazeti la Tanzania Daima mwaka 2011 na kesi hiyo ipo mbele ya hakimu mkazi Waliarwande Lema katika mahakama hiyo ya Kisutu?

Wanasiasa, na wanahabari mnaoijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama kuwa amebambikiwa kesi, mbona hamuonyeshi kuandika makala za aina hiyo za kusema nao wanabambikiwa kesi wakati kutwa mnafanya nao kazi miaka nenda rudi? Kuna nini hapa katika kesi ya Kaka yangu Lwakatare?Au kwasababu Lwakatare ni kiongozi wa kisiasa?

Napenda kuwashauri wale wote wanaoijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama kuwa hamsaidii Lwakatare isipokuwa maneno mnayoyatamka huenda yatazidi kumgandamiza kwa njia moja au nyingine. Sisi wasomi wa sheria tunasema hizo blah blah zenu hazina mashiko (merit).

Kwa kuwa mnadai Lwakatare amebambikwa kesi, ina maana mnaushahidi na hilo; Basi ili mumsaidie Lwakatare aepukane na balaa hilo.

Wanahabari ambao hata mlango wa mahakama ya Kisutu wala hata ya mashitaka ya kesi hiyo hamjaisoma wala kuiona, ni vyema mkaenda pale jengo la Sukari House, muombe kuonana na DPP-DkFeleshi na kisha mumueleze kwa vielelezo kuwa kesi hiyo ya PI 6/2013 R v Lwakatare, Ludovick ni ya kupikwa na ushahidi wa kuthibitisha hayo mmpatie.

Wanasiasa, hasa wabunge, mjirekebishe na mtambue kuwa porojo zenu mlizozoea kuzitoa majukwaani na kutoa ahadi za uongo kwa wananchi kupitia majukwaa ya siasa, hazikubaliki mahakamani hata chembe na wala mwisho wa siku haziwezi kuishawishi mahakama imuone mshitakiwa ana hatia au la. Mambo yanayohusu kesi mahakamani kwa taarifa yenu yanazingatia, sheria, kanuni na ushahidi, hizo porojo zenu wala mahakama haizitaki.

Lakini porojo hizi za wanasiasa hawa uchwara wanazozitoa katika kesi ya ugaidi ya Lwakatare, hazinishangazi kwani hata mwanasiasa mkongwe na msomi nchi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Sheikh Ponda alipofikishwa katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza na wenzake 49, Oktoba 18 mwaka jana, Lipumba alijitokeza hadharani katika mikutano yake na waandishi wa habari, tena bila haya, akaizungumzia kesi inayomkabili Sheikh Ponda --ambayo ni ya makosa ya  uchochezi wizi wa malighafi wa Sh. milioni 59 ambayo inatarajiwa kutolewa hukumu na hakimu Victoria Nongwa, Aprili 18 mwaka huu-- akasema kesi ni ya madai lakini anashangazwa na DPP kuifungua kuwa ni ya jinai. Sisi wasomi wa sheria tulimpuuza na niliandika makala ya kumpinga Lipumba iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho (PROFESA LIPUMBA NI MBUMBUMBU WA SHERIA).
Na Machi 4 mwaka huu, hakimu Nongwa alitoa uamuzi wake ambao alimuona Ponda na wenzake wana kesi ya kujibu na akatupilia mbali hoja ya wakili wa Ponda, Juma Nassor iliyokuwa ikidai kuwa kesi hiyo ni ya madai, ambapo hakimu alisema kesi hiyo siyo ya madai na kwamba kesi hiyo ni ya jinai.

Nihitimishe kwa kuwaasa wabunge wetu ambao mmeshupaza shingo kuijadili kesi ya Lwakatare nje ya mahakama, nanyi baadhi ya wanahabari wetu, kuwa sheria haina urafiki, na sheria ni msumeno. Mkae mkifahamu kuwa kufunguliwa kesi ni hatua nyingine, kukutwa na hatia au kuachiliwa ni hatua nyingine pia. Kwa hiyo Lwakatare yeye yupo kwenye hatua ya kufunguliwa kesi hiyo ambayo haina dhamana na bado hajatiwa hatiani; Hivyo ni vyema basi tuiachie mahakama, na mawakili wa pande zote mbili katika kesi hiyo ya mawakili wa utetezi na upande wa Jamhuri wafanyekazi yao ya kisheria ya kuisaidia mahakama mwisho ili mwishowe ifikie maamuzi ya haki.

Nina uzoefu mkubwa wa kuripoti kesi mbalimbali mahakamani kwa zaidi ya miaka 13 sasa. Nimejifunza kuwa ukiwa unashitakiwa ukae ukijua ndiyo umasikini umeukajiribisha ndani ya nyumba kwani utakimbiwa na marafiki na ndugu zako. Familia yako, na wale wa karibu, ndiyo watakaohangaika, wale uliokuwa nao wakati wa raha watakukumbia. Ndugu wa kaka yangu Lwakatare walitambue hilo.

Lwakatare alipokuwa hajakumbwa na matatizo ya kesi hii alikuwa anaheshimiwa na kuthaminiwa sana na muda wote watu walikuwa wakitaka kuwa naye karibu kwa ajili ya shughuli za kikazi, lakini si leo hii akiwa amepatwa na kesi hii.

Ndugu na jamaa wa kaka yangu Lwakatare nawataka mtege kuona watu hao wakiwa mbali kabisa na familia ya Lwakatare, wengine itafikia mahala mkiwapigia simu watakuwa hawapokei, hao ambao leo hii wanaojifanya wanaisemea kesi yake nje ya mahakama, mwisho wa siku watanyamaza kimya. Ndugu wa familia, msalaba wa majukumu ya kumpelekea chakula gerezani Kaka Lwakatare ni kwenu. Nashauri vyema muwakataze wote wanaotaka kuigeuza kesi ya ndugu yenu kuwa ni mtaji wao kisiasa, wakijipatia umaarufu wa chee. Tumieni muda mzuri wa kuwa karibu na mawakili wa Lwakatare. Puuzeni porojo za wanasiasa.  

Mwisho, baadhi ya  wanasiasa na wanahabari tuheshimu taaluma za watu wengine, yaani wanasheria, wapelelezi na mahakama. Na hiyo ndiyo dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka yaani (Separetion of Power).

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter