MSHAMBULIAJI wa Simba, Mrisho Ngassa, anafurahishwa na mashabiki wa Yanga kila wanapomshangilia.
Ngassa amekuwa akishangiliwa na mashabiki wa Yanga kila anapokuwa uwanjani akiichezea Simba, hali ambayo inaacha maswali mengi.
Wakati akiichezea Azam msimu uliopita, Ngassa alikorofishana na uongozi wa timu hiyo kutokana na kuibusu jezi ya Yanga. Sasa anasema anafurahia kushangiliwa na mashabiki wa timu hiyo.
Katika mchezo wa Jumapili iliyopita kati ya Simba na Coastal Union, Ngassa alitoka uwanjani (Taifa) huku akiwapigia makofi mashabiki wa Yanga, hali iliyowakwaza wale wa Simba.
Akizungumza na Championi Jumatano, Ngassa alisema anafurahia kupewa sapoti na mashabiki wa Yanga kwa kuwa anawachukulia kama Watanzania wengine tu ambao wameamua kumshangilia mtu wanayempenda.
“Mimi sioni kama kuna tatizo, kwani mtu yeyote ana uhuru wa kuchagua kinachomfurahisha na si kwa vile yuko upande tofauti,” alisema Ngassa.
Inadaiwa kuwa Ngassa ameshasaini mkataba wa kuichezea Yanga na ataitumikia timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake Msimbazi mwishoni mwa msimu huu.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....