KWELI kuelekea mwisho wa dunia, mengi yataonekana. Mtu unawezaje kumpiga shoka mama yako mzazi, aliyekutunza tumboni mwake kwa miezi tisa, akakunyonyesha, kukusomesha hadi kukua na kujitegemea?
Tukio zima, lilichukua nafasi Alhamisi iliyopita, Mtaa wa Malipula, Kata ya Chamwino, mkoani hapa na inadaiwa kwamba kabla ya mauaji, Hillary alimpiga vibao, mitama na mateke mama yake.
HALI HALISI ILIVYOKUWA
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Pili Athuman, alidai kwamba siku ya tukio, kulitokea mabishano kati ya Hillary na mama yake.
“Yalikuwa mabishano kidogo lakini ghafla yule kijana alimvamia mama yake na kuanza kumpiga,” alisema Pili na kuongeza:
“Yule kijana ni mtoto wa pekee wa yule mama. Tunashindwa kuelewa mpaka sasa chanzo cha tukio hilo. Halafu wale watu ni walokole kabisa na siku zote walikuwa wanaishi kwa upendo.”
Shuhuda mwingine, Julius Josephat alisema: “Mimi nashindwa kuelewa. Huyu marehemu na mwanaye walikuwa wanapendana sana, wakienda kanisani wanaongozana kama kumbikumbi.
“Kinachosikitisha zaidi ni kuwa mama yake aliumia mkono kama siku tatu kabla, akawa amefungwa plasta ngumu (POP), nahisi ndiyo maana alishindwa kujiokoa.”
Naye Maria Maswika ambaye nyumba yake imepakana na ile ya mama Hillary, alieleza: “Leo (Alhamisi), saa 4 asubuhi nilimsikia huyo mama akipiga kelele za kuomba msada, huku akiingia nyumbani kwangu.
“Nilipotoka chumbani, nilishuhudia kwa macho yangu yule kijana akimpiga shoka mama yake na kumuua palepale. Sababu ya ugomvi wao siielewi. Kwanza nashangaa sana, kwani yule mama wa watu alikuwa anampenda sana mtoto wake.”
HILLARY AKAMATWA
Mwandishi wetu alifika eneo la tukio mapema na kushuhudia wananchi wakimkamata Hillary, kumfunga kamba kabla ya polisi nao kuwasili, kuandika maelezo na kumchukua mtuhumiwa huyo wa mauaji ya mama yake mzazi.
RPC ANASEMAJE KUHUSU SHERIA?
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, ACP Faustine Shilogile, alisema: “Uchunguzi zaidi wa tukio unaendelea na utakapokamilika, tutamfikisha mtuhumiwa mahakamani.”
PAKA WA KUSHANGAZA
Kitu kilichowashangaza wengi eneo la tukio ni paka anayetajwa kumilikiwa na marehemu ambaye baada ya mama huyo kuuawa, yeye alikwenda kulamba damu kisha akalala kichwani kwenye mwili wa marehemu.
TUTAFUATILIA
Uwazi linaendelea kufuatilia na litaweka bayana sababu hasa ya mauaji hayo na kilichompata kijana huyo mpaka akachukua uamuzi wa kumuua mama yake.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....