MKALI wa Bongo Fleva, Hussein Machozi amelizwa vitu vyake mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato ‘laptop’ katika gesti aliyokuwa amefikia iitwayo Stanley mjini Singida.
Chanzo chetu makini kilichoomba kuhifadhiwa kilisema tukio hilo lilitokea Ijumaa Machi 8, 2013 katika gesti hiyo ambapo staa huyo alikwenda kufanya shoo na alipomaliza alipitia kwenye kikao cha kupanga mikakati ya shoo nyingine iliyoandaliwa na Seif Shabani ‘Matonya’.
“Aliporudi sasa ndipo akakuta vitu vyake havipo na maelezo ya wahudumu yalikuwa yanamchanganya tu ndipo akaamua kwenda polisi. Cha kushangaza aliporudi alikamatwa na kuwekwa ndani kwa maelezo kuwa alifanya vurugu kwenye sehemu ya biashara,” kilieleza chanzo hicho.
Kikaongeza: “Mmiliki wa gesti hiyo aitwaye Halingumu ndiye aliyempeleka ndani.”
Akifafanua juu ya tukio hilo, Hussein Machozi alisema: “Ni kweli hilo tukio lilitokea. Laptop yangu yenye thamani ya milioni mbili ilipotea hivihivi kaka. Kilichoniuma zaidi ni mimi kwenda kushitaki halafu narudi nakamatwa na kugeuziwa kibao.
“Nililala ndani usiku mmoja, nikaachiwa Jumamosi asubuhi (Machi 9, 2013) kwa kusingiziwa kufanya vurugu na kujeruhi, kitu ambacho si kweli.”
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....