ZIKIWA zimepita siku takriban tano toka kukutwa kwa mwili wa mtoto mchanga katika eneo la Semtema jirani na makazi ya wanafunzi wa chuo kimoja cha dini mkoani Iringa, simanzi na majonzi zimeendelea kutanda katika Manispaa hiyo baada ya mtoto mwingine wa jinsi ya kike kutupwa katika dampo la taka eneo la Stendi ya M.R mjini Iringa.
Wakizungumzia matukio hayo ya wanawake wasiofahamika kufanya vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto wanaowazaa, baadhi ya akina mama wamelitaka jeshi la polisi na jamii nzima kusaidiana kuendesha misako dhidi ya wanawake wanaofanya vitendo hivyo vya kikatili.
Sarah Sanga, mkazi wa Miyomboni mjini hapa alisema kuwa matukio ya wanawake kutoa mimba na kutupa watoto yameendelea na kuwa ni tishio katika Manispaa ya Iringa.
Bwana Said alishauri wanawake kuwafichua wenzao ambao siku za karibuni walionekana na mimba na ghafla mimba hizo kutoweka kwani wanaweza kuwa wahusika lakini akawalaumu wanaume kwamba wanaweza kuwa chanzo cha tatizo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk. Leticia Warioba akizungumzia tukio hilo amewataka mabinti na vijana wilayani hapo kuepuka kupeana mimba bila kuwa na uhakika wa ndoa.
“Serikali ya wilaya itaendelea kutoa elimu zaidi kwa vijana ili kupunguza tatizo la watoto kutupwa katika wilaya ya Iringa,” alisema
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, limethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kuahidi kuendelea na msako mkali ili kuwakamata wahusika.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....