MARA tu baada ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa 16 kutangaza Jumatatu wiki hii kuwa atajiuzulu Februari 28, mwaka huu kutokana na umri mkubwa na kukosa nguvu za kuendelea kuongoza, mjadala umeanza kuhusu ni nani atakayemrithi huku majina kadhaa yakiwekwa hewani.
Wachambuzi wa mambo ya kanisa hilo wanasema kuwa wakati umefika kwa Wakatoliki kupata Papa ambaye anatoka nje ya Bara Ulaya baada ya John Paul kutoka Poland na Benedict wa 16 kutoka Ujerumani.
Kiongozi mpya atapatikana mwezi ujao katika uchaguzi utakaofanyika makao makuu ya kanisa hilo jijini Vatican nchini Italia na utafanywa na makadinali kabla ya Sikukuu ya Pasaka.
Marekani ambayo ina asilimia 42 ya Wakatoliki wote duniani, inaona kuwa wakati umefika kwa kiongozi mpya wa kanisa hilo kutoka eneo hilo huku Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Sao Paolo, Odilo Scherer (63), akipewa nafasi kubwa ya kurithi kiti hicho.
Kutoka Afrika, Kadinali Peter Turkson (64) wa Ghana anayeongoza idara ya haki na amani katika kanisa hilo naye anapewa nafasi kubwa kuliwakilisha Bara la Afrika.
kutoka Afrika, mwingine anayetajwa ni Kadinali Francis Arinze (81) wa Nigeria.
Wengine wanaopewa nafasi ni Kadinali Angelo Scola wa Milan, Italia na Marc Oullete (68) wa Canada.
Kujiuzulu kwa kiongozi huyo kumekuja ghafla na kuwashangaza waumini wengi wa kanisa hilo duniani.
Papa Benedict, 85, alisema hawezi tena kuhudumu kama kiongozi wa kanisa hilo ambalo amekuwa akiliongoza tangu mwaka 2005 baada ya kufariki kwa Papa John Paul wa pili.
Kujiuzulu kwa kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki duniani ni jambo ambalo halijatokea kwa muda mrefu tangu miaka ya 1400, huku viongozi watano waliopita wakifia madarakani.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....