RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa mtindo wa kufanya fujo na kusababisha uvunjifu wa amani kwa visingizio vya dini nchini ni biashara inayolipa na ndiyo maana wakereketwa wa kufanya hivyo hawaishi.
Hata hivyo, akaonya kwamba Serikali katu haitawavumilia wanaotaka kuwavuruga Watanzania kwa kutumia dini zao.
Kikwete aliyasema hayo wakati wa kuwasilisha ripoti ya Mchakato wa Nchi za Afrika Kujitathmini zenyewe katika nyanja za Demokrasia, Utawala Bora na Uchumi (APRM) nchini Ethiopia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona kuwa wadau wanatumia dini kuiyumbisha nchi kwa vigezo kuwa ni miongoni mwa nchi zilizodumisha amani kwa muda mrefu.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali yake haitayumba wala kusita kupambana ipasavyo na wafanya fujo hao ikiwa ni pamoja na kutumia njia za busara wakati wa kutoa uamuzi na hatua za kisheria.
“Kuna baadhi ya watu wanatumia vigezo vya kidini kwa ajili ya kufanya vurugu za kuhatarisha amani, Serikali haitaweza kuwavumilia, badala yake tutatumia njia mbalimbali ili kushughulikia matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kutumia busara na hatua za kisheria,” alisema Kikwete.
Alisema mapendekezo yaliyotolewa na APRM ya kusimamia kwa uangalifu tofauti za kidini nchini ameyachukua kwa mikono miwili.
Alisema kitendo cha Tanzania kuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu ni bahati iliyotokana na kutokuwapo kwa ugomvi wa kikabila, kidini ama yale ya kutokana na rangi za watu. Alisema hali hii inatokana na ukweli kuwa sera iliyopo haina ubaguzi kwa wananchi kwa misingi ya kabila, dini, rangi ama sehemu anakotoka Mtanzania, ni sera nzuri na wanaidumisha.
Kwa mujibu wa Kikwete, uzuri kuhusu dini katika Tanzania ni kwamba kila mmoja ana uhuru wa kuabudu na kwamba Serikali haina dini.
“Tunajua fika kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini wenye malengo ya kuchochea fujo za kidini, hatuwezi kuyumba wala kusita kupambana ipasavyo na watu wa namna hiyo,” alibainisha.
Alisema ikiwa wataona uchochezi wa kidini unafikia kiwango cha kuhatarisha amani ya nchi ama uvunjifu wa amani na sheria na dola itachukua mkondo wake ili haki iweze kutendeka.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....