Mzimu wa Sharomilionea waanza kazi, wezi warudisha vifaa vyake

 
 
JESHI la Polisi mkoani Tanga limefanikiwa kukamata vitu mbalimbali vya marehemu Hussein Ramadhan, ‘Sharo Milionea’ vilivyoibwa na watu wasiojulikana, muda mfupi baada ya msanii huyo wa filamu na muziki nchini kupata ajali katika Kijiji cha Songa Kibaoni, wilayani Muheza na kufariki dunia papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Costantine Massawe alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata begi la nguo, simu ya mkononi aina ya blackberry, betri ya gari, redio, tairi la gari na saa ya mkononi ya marehemu.
Alitaja vitu vingine vilivyopatikana kuwa ni nguo ambazo marehemu alivuliwa baada ya kupata ajali, ambazo ni fulana na suruali ya jeans.
Alisema kuwa,vitu hivyo vilipatikana baada ya wakazi wa kijiji ilipotokea ajali hiyo kuvisalimisha vitu hivyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa kibaoni, Abdi Zawadi .
“Vitu viliwasilishwa na wasamaria wema kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa Kibaoni, Abdi Zawadi ambaye alitoa taarifa polisi kwa ajili ya utambuzi na taratibu nyingine,” alisema Massawe.
Aliwataka wananchi wa Kibaoni kuendelea kutoa ushirikiano ili viweze kupatikana vitu vingine vya marehemu na kuongeza kuwa, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, ili kubaini pesa na vitu vingine vilivyokuwamo ndani ya gari hilo ambavyo havikupatikana.
“Hivi vitu mnavyoviona hapa vimesalimishwa na watu ambao huenda walishiriki katika wizi, au waliviona mahali na kwa mapenzi yao kwa marehemu wakaamua kuvirejesha,” alisema Massawe
Alisema baadhi ya vitu hivyo vilikamatwa nje ya wilaya ya Muheza katika gereji na kwenye nyumba za watu.
Kamanda alifahamisha zaidi kuwa, hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kuhusika na tukio hilo.
“Tunaamini kuna vitu vingi vya thamani havijapatikana, bado tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wananchi na mtu atakayekutwa na kitu chochote cha marehemu atashtakiwa,” alisema Massawe.
Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa waliokutwa na vitu hivyo, lakini hakutaja idadi yao kwa kuwa vitu vingine havijapatikana.
“Pamoja na hayo, vitu vilikuwa vinasalimishwa usiku na wengine walivileta mchana kwa mwenyekiti wao. Hata hivyo, si kwamba mtu aliyeleta anakamatwa papo hapo, ila wale watakaokutwa navyo tutawakamata na kuwashtaki,” alisema Kamanda Massawe.
DC atoa neno
Awali Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu aliliambia Mwananchi kuwa, licha ya kusalimisha vitu hivyo hakuna mtu aliyekamatwa kwa sababu washukiwa bado wako mafichoni.
“Kwa kweli hadi sasa aliyekamatwa kwa sababu washukiwa wote wamejificha,”alisema Mgalu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kupatikana kwa vitu hivyo, kulitokana na amri aliyoitoa baada ya mazishi ya msanii huyo, kuwataka wakazi wa eneo ilipotokea ajali kuvirejesha vitu hivyo ifikapo Ijumaa saa 12.
“Nilikuwa kijijini Songa kibaoni hadi saa 5.30 usiku juzi (Jumatano) nikiwa sambamba na wakazi wa kijiji hicho ambao walipiga kura ya siri za kuwafichua waliohusika katika tukio hilo,” alisema Mgalu.
Aliwataka waliokimbilia mafichoni kurejea haraka watu wanaopatwa na ajali. Kwani lengo la Serikali ni kutaka wanaoishi kando ya barabara kuacha kuwafanyia unyama majeruhi na maiti mara zinapotokea ajali kwenye maeneo yao.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter