.
Polisi mkoani Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama wa chama hicho ndio waliohusika.
Polisi mkoani Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama wa chama hicho ndio waliohusika.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema amepinga kauli hiyo na kulipa jeshi hilo siku nne
kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa watano baada ya kulipatia majina hayo
akidai kuwa ndio wanaohusika na uchomaji moto ofisi za chama hicho.
“Tumewapatia polisi majina... tunaamini walihusika
moja kwa moja la sivyo, chama kitatumia vijana wetu wa Red Brigade
kuwakamata na kuwafikisha polisi,” Lema aliwaambia waandishi wa habari
jana.
Ofisi za Chadema zilizoko katika eneo la
Ngarenaro, zilinusurika kuteketea kwa moto juzi baada ya watu
wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya vyumba vyake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Japhet Lusinga alisema:
“Katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa hakuna
mahali palipovunjwa kutoka nje ya uzio na kuruhusu watu kuingia ndani...
tumegundua kuna tundu dogo darini eneo la kuelekea bafuni la upana wa
futi moja na nusu kiasi haliwezi kuruhusu mtu kupita.
“Tumejiridhisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupita hapo na ndani tulikuta majivu na baadhi ya vitu vilivyoungua na vifaa vingine.”
Lema akiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya
Arusha, Ephata Nanyaro alisema: “Tumebaini polisi wanataka kulifanya
jambo hili kama la siasa ndiyo sababu juzi badala ya kuanza kuchunguza
waliohusika, waliwakamata Mtunza Ofisi na mlinzi wetu na kuwalaza
rumande hadi leo (jana) asubuhi kwa madai eti wanawahoji.
“Hatukubaliani na taarifa yao, hii ni siasa.
Kulitokea mauaji ya bomu, wakasema Chadema wamejilipua, leo ofisi
imechomwa wanasema Chadema wenyewe, hili hatukubali, “ alisema.
Msajili alaani
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi amelaani tukio la kuchomwa moto ofisi hizo za Chadema na
kusisitiza kuwa wananchi hususan wanasiasa wasiwe wepesi kuingiza hisia
kwenye makosa ya kijinai.
Alisema kuwa tukio hilo linapaswa kukemewa kwa hali yoyote ile kwa kuwa linavuruga na kuhatarisha amani ya nchi.