KIJANA George Joseph wa Mwadui amekatwa mguu wake baada ya kupigwa risasi mwezi uliopita na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi walinzi wa mgodi wa Mwadui.
Kukatwa mguu huo kunatokana na madai kwamba mara baada ya kijana huyo kupigwa risasi, aliwekwa chini ya ulinzi bila kupelekwa hospitali kubwa hali iliyosababisha kuoza.
Joseph na watu wengine wanne walidaiwa kuingia mgodini isivyo halali Januari 9, mwaka huu na kukatokea vurugu ambazo zilisababisha kupigwa risasi na wengine wakashikiliwa na uongozi wa mgodi huo akiwemo yeye, jambo lililosababisha achelewe kupata matibabu hivyo mguu wake kuharibika na hatimaye kukatwa.
Kijana huyo alilazwa katika hospitali ya mgodi wa Mwadui tangu Januari 9, mwaka huu akiwa chini ya ulinzi wa askari lakini kukiwa hakuna huduma zilizokuwa zikitolewa jambo lililosababisha aombe kupewa rufaa bila mafanikio hadi
ndugu zake walipofanikiwa kumuondoa hospitalini hapo kwa kutumia nguvu na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini hapa ambako amekatwa mguu.
Joseph ameilalamikia serikali kwa kusema: “Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alikuwa ni mtu wa kwanza kumjulisha juu ya tukio hili na aliahidi kufika hospitalini lakini hakufanya hivyo hadi sasa nimeathirika na kuwa mlemavu kwa kukatwa mguu wangu.”
Kijana huyo alisema alishangazwa na ukimya wa polisi juu ya tukio hilo kwani kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga amekuwa akisema hana taarifa na tukio hilo wakati askari waliokuwa wamekuja siku ya vurugu walitoka mkoani Shinyanga na walichukua maelezo yake.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, ACP Evarist Mangala alipotafutwa kujibu malalamiko juu ya tuhuma hizo, alisisitiza kwamba hana taarifa lakini akamshauri mgonjwa aandike barua ya malalamiko juu ya tukio hilo ili aweze kulifanyia kazi.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....