MFANYAKAZI wa ndani aliyetambuliwa kwa jina la Mwantumu Hassan (22) amekutwa amekufa ndani ya kisima, huku akiwa ameacha ujumbe wa "Mwantumu A Hassan najua kitakuwa kilio kwetu, mniombee nifike niendako mwisho wa kuishi duniani".
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, tukio hilo ni la juzi sa 3:00 usiku katika maeneo ya Mbezi Juu, Goba kwa Mloa.
Alisema kwa mujibu wa mtoa taarifa Manara Kakwezi (28), mfanyakazi huyo wa ndani hakuonekana maeneo ya nyumbani kwa muda mrefu, jambo lililowatia wasiwasi na kuamua kuanza kumtafuta.
“Walimkuta katika kisima cha maji safi ambayo ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku akiwa ameshakufa,” alisema kamanda.
Mara baada ya kufanya upekuzi katika vitu vyake ndipo ulikutwa ujumbe huo katika pochi yake.
Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo chake, maiti imehifadhiwa hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
Katika tukio jingine, mpanda minazi aliyetambuliwa kwa jina la Ally Ramadhani (50) amekufa papo hapo baada ya kuanguka kutoka kwenye mnazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema mtu huyo aliteleza na kuanguka na kufa papo hapo.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....