MKAZI wa Makongorosi, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Januari Juma (30), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko12 baada ya kupatikana na kosa la ujambazi wa kutumia silaha.
Adhabu hiyo iliyotolewa baada ya Juma kukiri mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, kutenda kosa la kupora pikipiki, simu ya mkononi na fedha taslimu sh 45,000.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka, Thomas Kilakoi, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 6 mwaka huu, akiwa na wenzake wanne, Frank Peter, George Lwanji, Hussein Feli na Ericko Sikujua.
Alidai kuwa kwa pamoja washtakiwa walimvizia njiani Aggrey Mwezimpya mkazi wa kijiji cha Mkusi na kumpora vitu hivyo baada ya kumtishia kumkata kwa mapanga.
Mbele ya Hakimu Adamu Mwanjokolo, Kilokoi aliendelea kudai kuwa baada ya kumpora Mwezimpya vitu hivyo saa moja jioni, watuhumiwa waliondoka na kukimbilia katika kijiji cha Mwaoga wilayani Chunya ambako walikamatwa na polisi wakiwa na pikipiki hiyo.
Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, Juma alikiri kutenda kosa hilo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 huku wenzake wanne wakikana mashtaka na kurejeshwa mahabusu hadi kesi yao itakapotajwa tena.
Mwandishi ni Sammy Kisika, Sumbawanga
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....