Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, alisema watuhumiwa hao walikamatwa usiku huo huo katika maeneo tofauti ya mji wa Tanga.
Massawe alisema polisi inawahoji watuhumiwa waliokamatwa, ili kubaini wahusika halisi wa tukio hilo, kabla ya kuwafikisha mahakamani.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, Polisi pia inachunguza tukio jingine la kutaka kuchoma moto Kanisa la Miracle Revival, lililoko katika mji wa Makorola.
Usiku wa kuamkia juzi, watu wasiojulikana walijaribu na kuchoma moto makanisa mawili, banda moja la kuoneshea picha za video na banda la pombe za kienyeji, na kusababisha hofu ya uhalifu dhidi ya dini ya Kikristo kuenea miongoni mwa wakazi mkoani hapa.
Siku hiyo saa 8 usiku, Kanisa la Betham lililokuwa likitumika zamani, liliteketezwa kwa moto na baada ya hapo watuhumiwa waliingia ndani ya kanisa kubwa la sasa, na kuchoma moto vitambaa vilivyofunika madhabahu.
Pia, usiku huo huo saa 9, Kanisa la Miracle Revival lililopo eneo la Makorola, lilinusurika kuchomwa moto baada ya juhudi hizo kuzimwa na watu waliojitolea kuuzima, wakati ulipokuwa umeshawashwa kwenye nguzo za kanisa hilo.
Wakati huo huo, Polisi mkoani wa Mbeya, inamshikilia mkulima Emmanuel Mlagala (28) kwa tuhuma za kumpiga na kumsababishia kifo Faustino Lulambo (55), katika eneo Madibila, Mbarali Jumatano iliyopita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Diwani Athumani, alisema ugomvi huo ulitokea katika mashamba ya mpunga saa nne asubuhi, na Faustino alikufa kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Alisema kabla ya kifo, kuliibuka ugomvi baada ya Mlagala kutuhumiwa kuiba simu, ambayo thamani yake haijajulikana. Polisi bado wanaendelea kuchunguza chanzo cha tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....