Rais Jakaya Kikwete (katikati) akishikana mikono na viongozi wengine kuimba wimbo wa Mshikamano Daima wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya jana.
 


Wafanyakazi nchini watapata nafuu kimapato, pale Serikali itakapoanza kutekeleza azma yake ya kupunguza kodi kwenye mishahara (PAYE) wiki mbili zijazo.

Rais Jakaya Kikwete, jana aliashiria hivyo baada ya kutangaza punguzo la PAYE, kwa lengo la kupunguza mzigo wa ugumu wa maisha kwa mfanyakazi.
 


Alitangaza hatua hiyo alipohutubia wananchi jana katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, yaliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari.
 


“Tangu mwaka 2007 baada ya kilio cha wafanyakazi, tulipunguza kodi kutoka asilimia 18 hadi 15, na kwa mwaka 2010/11 tulipunguza hadi asilimia 14.
 


“Februari mwaka huu tulipokutana na viongozi wa chama cha wafanyakazi, tulizungumzia hili la kupunguza kodi ili kutoa nafuu kwa wafanyakazi. Waziri wa Fedha atakaposoma Bajeti yake wiki mbili zijazo, atatangaza punguzo hilo la kodi,” alisema Rais Kikwete.
 


Kuhusu nyongeza ya mishahara, Rais alielezea mafanikio ya Serikali tangu alipoingia madarakani, ambapo alikuta kima cha chini kwa mfanyakazi kikiwa Sh 65,000 na kupandisha kila mwaka hadi Sh 170,000.
 


Aliahidi wafanyakazi wote nchini, kwamba Serikali itaendelea kuongeza mishahara kulingana na hali ya uchumi wa nchi.
 


Akifafanua suala la nyongeza ya mishahara ambalo ni kiu kubwa kwa wafanyakazi, Rais alisema pamoja na Serikali kupenda kuongeza mishahara kwa wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha, lakini lazima izingatie hali ya mapato yake.
 


Alisema Serikali imekuwa ikitumia asilimia 44.9 ya mapato ya ndani kulipa mishahara pekee, bila kujumuisha mahitaji mengine ya maendeleo.
 


Alisisitiza kuwa pamoja na nia nzuri ya kutaka kuongeza mishahara, lazima uwepo uwiano wa mzuri kati ya ulipaji wa mishahara na utekelezaji wa majukumu mengine ya maendeleo sambamba na ukuaji uchumi.
 


“Watu wakiona kuwa hatuwezi kuongeza mishahara kama wafanyakazi na Serikali wangependa iwe,  wasidhani kuwa Serikali haipendi au tuna roho mbaya na wengine - mtimanyongo, bali uwezo ndio unaozuia kufanya hivyo,” alisema.


Kuhusu deni la Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali (PSPF), Rais Kikwete alisema hakuna mwanachama wa Mfuko huo atakayestaafu bila kupewa mafao yake.
Mwaka 1999 Serikali iliamua kuunda PSPF na kuachana na mtindo wa kulipa pensheni kutoka kwenye bajeti.


Kutokana na hilo, alisema Serikali ilitakiwa kulipa michango ya wanachama ya miaka ya nyuma, ambayo kimsingi ilitakiwa kulipwa na Serikali kama mwajiri na mfanyakazi, kabla ya kuanza kwake na sasa deni hilo limefikia Sh trilioni 6.4.
 


“Pamoja na hali ya Mfuko huo kuwatia hofu wanachama wake, lakini niwahakikishie kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu kwani hakuna mwanachama atakayestaafu bila mafao yake, hata kama mafao ya mfanyakazi yatafikia zaidi ya Sh bilioni 50,” alisema.
 


Alisema hali kama hiyo iliukuta Mfuko wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF),  lakini Serikali ilikubali kutoa Sh bilioni 50 kila mwaka kwa ajili ya Mfuko huo, ambao kwa sasa umefikia hatua nzuri. Alisema juhudi hizo pia zitafanywa kwa PSPF.
 


Kuhusu deni la wafanyakazi linalotokana na malimbikizo ya nyongeza za mishahara, posho za kuhama na nyinginezo, Rais Kikwete alisema serikali itahakikisha wafanyakazi hao wanalipwa malimbikizo ndani ya muda mfupi ujao.
 


Alisema wataendelea na utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na Chama cha Waajiri (ATE) katika kuzungumzia maslahi ya wafanyakazi.


Rais Kikwete aliendelea kusisitizia Watanzania juu ya kudumisha umoja na mshikamano wao bila kujali tofauti za dini, na kuwa mifarakano ya kidini itaipeleka nchi pabaya.
 


Alisema tayari ameshakutana na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, ambao wote wamekubali kuwa uhusiano wa waumini wa dini hizo mbili unakokwenda si kuzuri.
 


Kwa mujibu wa Rais Kikwete, utaratibu unaandaliwa wa kukutanisha viongozi hao wote na Serikali, ili kujadili namna ya kurejea katika uhusiano uliokuwapo kabla ya kuibuka kwa hisia za chuki.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter