MWAKA MMOJA WA KIFO CHAKE…KANUMBA ANAKOSESHA WENGI USINGIZI!

Steven Kanumba akiwa katika pozi enzi za uhai wake.
Tulipoteza mtu aliyekuwa amefungua milango ya kuajiri watu wa rika mbalimbali, hasa vijana kupitia filamu za nyumbani Tanzania. Alikuwa na kipaji kikubwa cha uigizaji. Katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, mwezi mmoja kabla ya kifo chake, nje ya Ofisi Kuu ya Global Publishers, Bamaga-Mwenge, Dar, Kanumba alithibitisha kwamba ataitangaza tasnia ya filamu za Kibongo duniani kote.
Tayari alikuwa ameweka mizizi huko Nollywood, Nigeria, Gollywood, Ghana, Hollywood, Marekani, Uingereza, Rwanda, Burundi, Congo na sehemu nyingine duniani.  Kuna ushahidi kuwa alikuwa amesaini mkataba wa kufanya filamu huko Hollywood ambayo ingempa utajiri mkubwa kuliko staa yeyote Afrika Mashariki. Kibaya aliondoka mapema kwa kuwa kizuri hakidumu. Kama Kanumba angekuwa hai, naamini filamu za Kitanzania zingekuwa mbali sana kimataifa.

Kanumba akiwa na rafiki yake Patcho Mwamba.
Ni Kanumba aliyewashawishi na kuwaingiza vijana wengi katika tasnia hiyo. Akina Wema Sepetu, Patcho Mwamba, Shamsa Ford, Kajala Masanja na wengine wengi ni mashuhuda. Kuna kila sababu ya kumuenzi Kanumba aliyefariki akiwa na umri mdogo wa miaka 28 tu.
Usiku wa kifo cha Kanumba haukuwa mzuri hata kidogo kwa watu wengi. Habari zilisambaa kama moto wa kifuu hasa kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na simu za mkononi. Kila mtu alibisha. Wengine walidhani ni sehemu ya filamu zake. Hata hivyo, baadaye madaktari wa Muhimbili walithibitisha kifo chake. Kibaya zaidi, kifo chake kilihusishwa na mwigizaji kinda, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye alikamatwa na kuwekwa katika Mahabusu ya Segerea, Dar kabla ya hivi karibuni kutoka kwa dhamana na kesi inatarajiwa kuanza kuunguruma muda wowote.
Kanumba alipendwa na bado anapendwa majumbani hasa wanawake na watoto. Kilipotangazwa kifo chake mwanamke mmoja alikunywa sumu huko mkoani Pwani. Watoto walimlilia kwa sababu ya aina ya filamu alizoigiza zilizogusa maisha yao. Alikuwa kipenzi cha watoto.

Steven Kanumba akiwa na Jack Wolper wakati wakiandaa filamu ya 'Ndoa Yangu'.
Kifo chake kiligusa hisia za wengi wakiwemo wanasiasa, viongozi wa serikali, mastaa na watu wa kada mbalimbali nje na ndani ya Tanzania ambao walituma salamu zao za rambirambi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliyefika nyumbani kwa staa huyo Sinza ya Vatican Hotel, Dar wakati wa msiba.
Usiri wa maisha binafsi, hata lile la uhusiano wake na Lulu, upembuzi wa mambo, kujituma katika kazi, ushawishi, kutokuwa na majivuno na upole, ni vitu vinavyoigwa kutoka kwake hasa na wasanii wenzake.
Kuanzia akiigiza tamthiliya akiwa Kaole Sanaa Group hadi akaingia kwenye filamu, nyota yake ilikuwa iking’aa hata kama kipato hakikuwa kikubwa. Msanifu kurasa wa Global Publishers, Huruma Bujiku huwa analengwalengwa na machozi kila anapotengeneza kurasa zinazohitaji matumizi ya picha za Kanumba.

Kanumba akiwa na tuzo za Muigizaji bora wa Filamu pamoja na Mtayarishaji bora wa filamu 2010.
Unajua kwa nini hasahauliki? Bado filamu zake zinatazamwa sana majumbani mwetu zikishindana na zile za akina Jacob Steven ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter