Hatimaye jeshi la Polisi linamshikilia mwanaume anayetuhumiwa kumnajisi, kumbaka na kumlazimisha kula mbegu zake za kiume binti yake wa kambo.
Mwanaume huyo, Adam Tuliani, maarufu kwa jina la Kiredio (37) mkazi wa kijiji cha Mwandege, Wilaya ya Mkuranga, anadaiwa kumfanyia unyama huo mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka tisa .
Akitoa taarifa hiyo, Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi Vikindu, Inspekta wa Polisi Bahati Ponela alisema kupatikana kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na juhudi zilizofanywa na Mkuu wa kituo hicho, Inspekta Joseph Ndifwa na wananchi wa eneo hilo.
"Polisi imemkamata mtuhumiwa leo (jana) baada ya juhudi kubwa ya kumsaka iliyoongozwa na Mkuu wa kituo baada ya kuwa mafichoni kwa wiki moja," alisema inspekta Bahati.
Hata hivyo, Inspekta bahati alisema tukio la mtoto huyo kufanyiwa ukatili huo kwa miaka miwili mfululizo, halikuwahi kuripotiwa kwenye kituo na kusababisha mtuhumiwa kutokamatwa haraka.
"Hakuna mtu aliyekuja hapa kuripoti katika kipindi chote hicho kama ilivyoelezwa, jambo hili baya na mkuu wangu asingesita kuchukua hatua za haraka za kumkamata mtuhumiwa kama ilivyofanyika sasa," alisema Inspekta bahati.
Awali ilibainika mtoto huyo alifanyiwa vitendo hivyo kwa miaka miwili mfululizo kuanzia mwaka 2011 hadi mwanzoni mwa mwaka huu.
Wakati mtuhumiwa huyo akishikiliwa na polisi, imethibitika mtoto aliyefanyiwa unyama huo ameambukizwa virusi vya Ukimwi na ana matatizo ya kutokwa na haja sehemu zote za siri bila mwenyewe kujitambua.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, mama mdogo wa mtoto huyo, Chiku Selemani, alisema kwenye vipimo alivyofanyiwa katika Hospitali ya Mkuranga imeonyesha mtoto huyo ameambukizwa virusi vya Ukimwi na sehemu zake za siri zimeharibiwa kiasi cha kusababisha haja kutoka bila kujitambua.
Awali, mtoto huyo alieleza jinsi alivyokuwa akilazimishwa kula mbegu hizo kila siku wakati baba yake huyo alipomaliza kufanya mapenzi na mama yake mzazi na baada ya kumuingilia yeye.
Alisema wakati anafanyiwa vitendo hivyo, mama yake alikuwa akishuhudia na wakati mwingine alimsihi asikatae kwa sababu watakosa chakula.
KITONGOJI CHAPIGWA BUTWAA
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwandege, Abdallah Ngumbule alisema walikuwa hawatambui kama mtoto huyo aliyeonekana kurandaranda mitaani alikuwa akifanyiwa vitendo hivyo vya kikatili.
Ngumbule alisema ofisi yake ilitambua kuwapo kwa hali hiyo kupitia vyombo vya habari, na haraka walianza kushirikiana na polisi kumtafuta mtuhumiwa na mke wake ambao wote walikuwa wametoroka.
"Huyu mtoto tulikuwa tunamuona akizurura mitaani, lakini hatukujua kama anakimbia mambo machafu ya baba yake. Tulipobaini jambo hili tuliungana na polisi kuwatafuta mtuhumiwa ili akamatwe," alisema
MAMA AOMBA MSAADA
Hata hivyo, Chiku ambaye ni mama mdogo wa binti huyo ameomba kusaidiwa katika kumtunza baada ya hali yake kuwa mbaya kiuchumi.
Alisema madaktari wamemtaka kumpeleka mtoto huyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu kila mara, kitu ambacho alisema hataweza kwa kukosa pesa za nauli.
"Maisha yangu magumu, sina kitu chochote cha kuniingizia kipato, naomba Watanzania wenzangu wanisaidie katika jambo hili," alisema Chiku.
Kwa mtu atakayeguswa na tukio hili na kutaka kutoa msaada wake, awasiliane kwa kutumia namba za simu 0717336368, 0767377080 au 0683336368 au afike ofisi za The Guardian.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....