MKAZI wa Kijiji cha Mrito, Kitongoji cha Nyabihero, Kata ya Kwamambo Tarafa ya Ingwe, Wilaya ya Tarime mkoani Mara , Ryoba Marwa (75) anadaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mikononi mwa polisi.
Mke wa marehemu akiwa na wajukuu zake.
Habari kutoka katika Kituo cha Polisi cha Bibacho, Tarime zinadai kuwa mzee huyo alijinyonga kwa kamba ya jaketi lake akiwa mahabusu.Mtuhumiwa huyo inaelezwa kwamba alikamatwa nyumbani kwake Desemba 19, mwaka jana akiwa anatoka katika sherehe za vijana wa ndugu zake waliokuwa wametahiriwa.
Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kuwepo kwa mvutano mkubwa baina ya familia ya marehemu na jeshi la polisi kwani ndugu wanadai mzee wao aliteswa na tayari wameandika barua kwa Mkuu wa Wilaya, John Henjewele kulalamikia kifo hicho.
Kufuatia utata huo, mwandishi wa habari hii alikwenda Kijiji cha Mrito ili kujua ni kitu gani kilichosababisha mzee huyo kukamatwa na kutupwa mahabusu na kufia huko.
Mke wa marehemu, Mgaya Ryoba (56) aliyeshuhudia mumewe akikamatwa, alikuwa na haya ya kusema: “Nakumbuka siku hiyo ilikuwa saa 7.00 mchana , nikiwa nyumbani niliwaona polisi watatu wenye bunduki kila mmoja huku wakiwa na pikipiki mbili, walimzingira mume wangu wakamweleza kuwa anauza bangi hivyo yupo chini ya ulinzi.
“Marehemu alitii amri akawaambia kwamba yeye hafanyi biashara hiyo na kama walikuwa na wasiwasi wakague kila sehemu, wakakagua kila chumba na kwenye maghala hawakupata bangi.
Wajukuu zake walipoona babu yao anaondoka na polisi walilia sana na kesho yake Desemba 20,nilimpelekea chakula huko kituoni, nilizungumza naye akaniambia anaumwa kifua.
“Nilimuuliza kama polisi walimpiga akasisitiza tu kwamba anaumwa kifua na alikuwa akitokwa na machozi. Akasema askari wanahitaji shilingi 200,000 ili wamuachie, hivyo alinitaka niende nyumbani nikawaambie ndugu zake wakusanye hizo fedha zipelekwe ili aachiwe.
“Nilipofika nyumbani nilimweleza mtoto wetu wa kwanza Chacha Ryoba ambaye hakukubaliana na dai hilo na Desemba 21 alikwenda kituoni kujua hizo fedha ni za nini,”alisema mama huyo.
Chacha alipohojiwa alisema alipofika kituoni aliwauliza polisi alipo baba yake ambapo walimweleza kuwa alikuwa akijisikia vibaya hivyo wamempeleka hospitali lakini alipompigia simu mkuu wa polisi wa wilaya, (OCD) alimueleza kwamba baba yake alifariki baada ya kujinyonga kituoni .
“Nilijisikia uchungu kufuatia taarifa hizo za kutatanisha, nilijiuliza iweje baba ajinyonge hadi kufa wakati watuhumiwa hawaruhusiwi kuingia na kitu chochote mahabusu, kwanza baba alikua amevaa shati hilo jaketi alilitoa wapi? Inawezekana alipigwa hadi kufa, ninashangazwa pia kwa kitendo cha kuwahamisha kituo polisi waliokuja kumkamata wakapelekwa Kituo cha Nyamwaga. Naomba polisi watuonyeshe hizo bangi alizokamatwa nazo baba,” alisema Chacha.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime Rorya, ACP Kamugisha alipoulizwa kuhusiana na kifo hicho alisema marehemu alitumia kamba ya jaketi lake kujinyonga na uchunguzi unaendelea.
Marehemu alizikwa Desemba 22, mwaka jan
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....