Manumba ambaye yupo kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, mabadiliko ya afya yake yamekuwa na mshangao wenye masikitiko kwa familia yake, jeshi la polisi na serikali kwa jumla.
Udadisi uliofanywa na Uwazi, umebaini kuwa sababu kubwa ya mshangao huo ni ukweli kwamba Manumba aliuanza mwaka huu akiwa mwenye afya njema mpaka ilipofika Januari 10.
Vyanzo visivyo na shaka ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, vinasema kuwa bosi huyo nambari mbili baada ya IGP, mara yake ya mwisho kufika ofisini ni Alhamisi ya Januari 10, mwaka huu.
“Siku hiyo alionekana mwenye afya njema, alifanya kazi zake vizuri kama kawaida yake. Unajua yule bosi wetu ni mpiganaji sana,” alisema mtoa habari wetu, aliye makao makuu ya jeshi la polisi.
HISTORIA YA UGONJWA WA MANUMBA
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, hali ya Manumba ilianza kubadilika usiku wa Januari 10, mwaka huu, hivyo kumfanya siku iliyofuata, asifike kazini,
JANUARI 11 (Ijumaa): Manumba alipumzika nyumbani kwa sababu alikuwa anajisikia vibaya. Hatujapata uthibitisho kama siku hiyo alikwenda hospitali.
JANUARI 12 (Jumamosi): Manumba alikwenda hospitali moja jijini Dar es Salaam (haijatajwa), huko alikwenda kufanyiwa vipimo baada ya kuona hali yake inazidi kubadilika.
“Mwanzoni alihisi ni uchovu tu, kwa hiyo alipoona hali inazidi kuwa mbaya ilibidi aende hospitali kufanyiwa vipimo vya uhakika,” alisema mtoa habari wetu.
JANUARI 13 (Jumapili): Hali ilikuwa mbaya zaidi, akakimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa.
JANUARI 14 (Jumatatu): Vipimo vilionesha ana wadudu wengi sana wa malaria (zaidi ya wadudu 500), vilevile akakutwa na matatizo ya figo.
Siku hiyohiyo, alihamishiwa Hospitali ya Aga Khan ambako kuna mashine maalum ya kuzisaidia figo kufanya kazi.
JANUARI 15 (Jumanne): Taarifa rasmi kuhusu hali ya Manumba ilifikishwa Ikulu na kumshtua Rais Jakaya Kikwete.
JANUARI 16 (Jumatano): Rais Jakaya Kikwete, alifika kwa mara ya kwanza Hospitali ya Aga Khan kumuona DCI Manumba.
Januari 17 (Alhamisi): Rais Kikwete alikwenda kumuona Manumba kwa mara ya pili, hali aliyomkuta nayo, ilimfanya JK aondoke viunga vya hospitali hiyo akiwa mnyonge.
JK, aliingia wodini akiongozana na IGP, Said Mwema huku sura zao zikiwa zimechangamka lakini baada ya kutoka, kiongozi huyo wa nchi alikuwa mnyonge mno.
Siku hiyohiyo, mke wa rais, Mama Salma Kikwete na makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi, Dar es Salaam, walikwenda kumuona Manumba.
JANUARI 18 (Ijumaa): Zilivumishwa habari za uongo kwamba Manumba amefariki dunia.
JANUARI 19 (Jumamosi): IGP Mwema alisambaza taarifa kwa makamanda wote wa polisi nchi nzima, akiwathibitishia kwamba Manumba hajafa, na anaendelea na matibabu.
IGP aliandika: “Makamanda wa polisi wa mikoa, nawataarifu DCI Robert Manumba ni mgonjwa, anaendelea na matibabu, taarifa za uvumi kwamba amefariki si za kweli, anaendelea kupata matibabu, tafadhali wajulisheni wakuu wa vikosi na askari wasiwe na wasiwasi.”
JANUARI 20 (Jumapili): Ilielezwa kuwa Manumba anaendelea na matibabu, akisaidiwa kupumua kwa mashine ya oksijeni. Ikaelezwa pia kuwa hawezi kuzungumza na hatambui chochote.
JITIHADA ZA KUMPELEKA NJE
Kutokana na hali ya Manumba, kumekuwa na shinikizo la kumpeleka nje ili apatiwe matibabu zaidi lakini kumekuwa na ugumu kwa sababu hatua aliyonayo kwa sasa, kitaalamu haimruhusu kusafirishwa.
Chanzo chetu kilisema: “Alitakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini ilishindikana kwa sababu hajitambui, wakajaribu kumzindua, ikashindikana.”
WATANZANIA WAMTAKIA KILA LA HERI
Habari za ugonjwa wa Manumba, zimetikisa nchi hasa wiki iliyopita, kutokana na hali hiyo, ndani ya mitandao ya kijamii, watu mbalimbali walitoa maoni yao.
Katika maoni hayo, kubwa zaidi ni kwamba Watanzania wanamtakia kila la heri katika matibabu yake na kumuombea apone haraka.
POLISI NI MASIKITIKO
Kwa mujibu wa bosi mmoja ndani ya jeshi la polisi aliyeomba hifadhi ya jina lake, hali ya Manumba inawaumiza kwa sababu ni kiungo mzuri sana kazini.
“Yule jamaa ni mchapakazi. Tumwite jembe. Anasaidia sana. Sisi tunaofanya kazi chini yake tunajua ni jinsi gani alivyo jembe,” alisema bosi huyo wa polisi.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....