WATU wawili mkoani Singida wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mtoto mwenye umri wa miezi minne kupoteza maisha baada ya kukeketwa.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sizumwa alimtaja mtoto aliyefariki dunia baada ya kukeketwa kuwa, ni Shamila Saidi.
Alisema tukio hilo la kinyama lilitokea Oktoba 27, mwaka huu saa 10:00 alfajiri Kijiji cha Mwanyonyi, Tarafa ya Ilongero, mkoani Singida.
Alisema siku ya tukio, mama mzazi wa mtoto huyo alimpeleka mtoto wake kukeketwa kwa ngaraiba, ili aweze kupona ugonjwa wa kuharisha na kutapika. Magonjwa hayo yanadhaniwa kusababishwa na ugonjwa wa lawalawa.
Sizumwa alisema baada ya kukeketwa, mtoto huyo alivuja damu nyingi na kusababisha kifo chake.
“Hadi sasa tunamshikilia mama yake na watu wengine wote wakazi wa Kijiji cha Mwanyonye. Ngariba alifanikiwa kutoroka lakini tumeanzisha msako mkali kumkamata ili tuwafikishe kwenye mahakamani,” alisema.
Katika hatua nyingine, Sizumwa alisema Samwel Majilala mkazi wa Kijiji cha Kideka, Kata ya Puma, Wilaya ya Ikungi ameuawa na vijana wenye hasira kwa kinachodaiwa ni kumpiga baba yake mdogo.
Alisema mauaji hayo yamechangiwa na ugomvi wa kugombea Sh600,000 ambazo babu yake alilipwa fidia ya kupisha ujenzi wa umeme wa upepo.
“Katika fidia hiyo, mtoto alipata mgawo wa Sh200,000. Mjukuu wa mzee naye alianza kuomba kupewa mgawo. Samwel baada ya kushindwa kupata mgawo huo alianza kumpiga baba yake kwa madai kuwa ni kikwazo cha yeye kukosa,” alisema.
Alisema Samwel baada ya kumpiga baba yake mdogo, alitoroka na kukimbilia Kijiji cha Dung’unyi ambako alifuatwa na kundi la vijana na alipokamatwa, alipigwa hadi kusababisha kifo chake.
Kamanda Sizumwa alisema hadi sasa wanawashikilia watu saba kuhusiana na mauaji hayo na msako zaidi unaendelea.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....