KATIBA YAMVURUGA RAIS KIKWETE....WAPINZANI WAMPA MASHARTI MAZITO KUKUTANA NAE KABLA YA TAREHE 10....



SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuvisihi vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kusitisha maandamano yao na kurejea meza ya mazungumzo ili kupata muafaka wa muswada wa sheria ya kubadili sheria ya mabadiliko ya katiba, vyama hivyo vimetoa masharti mazito ya kukutana naye.

Hatua hiyo inakuja wakati vyama hivyo vikiendelea kushikilia msimamo wao wa kuitisha maandamano ya nchi nzima kupinga muswada huo, wanaodai kuwa unalenga kuipa CCM nafasi ya kuhodhi mchakato wa katiba mpya.

Wakati vyama hivyo vikiwa vimefanya mikutano ya ndani na makundi mbalimbali, na kisha mikutano miwili ya hadhara Dar es Salaam na Zanzibar, CCM nayo inakazana kumshinikiza rais asaini muswada huo kama ulivyopitishwa na Bunge.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwepo mvutano mkali ndani ya CCM, ambako makundi ya vigogo wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015, wanampinga Rais Kikwete kwa jinsi anavyoendesha mchakato huo, wakidai anawabeba wapinzani.
 
Licha ya wadadisi wa masuala ya kisiasa kumtabiria Rais Kikwete kuwa anaweza kujiandikia historia nzuri endapo mchakato huo ukifanikiwa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi, CCM inamtazama mwenyekiti huyo kama anataka kuwakomoa wenzake.
 
“Kuna msuguano mkali ndani ya CCM, Rais Kikwete ana nia njema na mchakato huu ili ukamilike kwa amani, lakini wenzake ndani ya chama wanadhani anataka kuwanufaisha wapinzani kwani hatakuwa na chochote cha kupoteza,” alisema kigogo mmoja wa CCM.
 
Ni katika nia njema hiyo Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, aliwasihi viongozi wa vyama vitatu vya upinzani kutoandamana, badala yake wakae na kutafuta njia mbadala ya kisheria kuboresha muswada huo, na kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
 
Hata hivyo, wito wa Rais Kikwete umepokelewa kwa taswira tofauti na vyama hivyo, vikisema kuwa yeye ndiye anapaswa kuwaandikia barua kuwaomba akutane nao kwa mazungumzo Ikulu, kwani wao hawajawahi kuomba kukutana naye.

Badala yake, vyama hivyo vilisisitiza kuwa viliomba kukutana na wadau mbalimbali na wananchi kumshinikiza asisaini muswada, na kwamba msimamo wao uko pale pale.

Katika msimamo huo, vyama hivyo vimesema maandamano yaliyotangazwa kufanyika Oktoba 10 nchi nzima yako pale pale, na kamati ya maandalizi inaendelea kufanya taratibu zote.
 
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam, wawakilishi wa vyama hivyo, John Mnyika (CHADEMA), Faustine Sungura (NCCR-Mageuzi) na Abdul Kambaya (CUF), walisema kuwa kamati ya maandalizi ya maandamano inaendelea kwa kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake hakugusia suala lolote kama atasaini muswada huo au la.
 
“Rais amezungumzia hoja za upinzani za kuvunjwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba kabla ya kumaliza muda wake, kwa hili tunampongeza, amekuwa wazi. Lakini afahamu kuwa hiyo si hoja kuu iliyosababisha tuandae maandamano kushinikiza asisaini huo muswada.
 
“Mambo mengine mazito yapo, kuhusu muundo wa Bunge la Katiba na idadi ya wajumbe kwa uwiano sawa wa Zanzibar na Tanganyika na kuhusu maoni ya wadau kuachwa,” alisema Mnyika.

Alisema kuwa maoni ya wadau yamepuuzwa, uchakachuaji umefanyika, taasisi zilipeleka majina, lakini Rais Kikwete anasema kuwa alizingatia hilo, kwamba wanamwomba aseme kwanini hakuchukua jina kati ya yale yaliyopendekezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu (Shiwavyata) na CCT.
 
Alisema kuwa hao walijitokeza kwenye kamati wala hawakusema kwa siri, hivyo Rais Kikwete awaambie mawaziri wake wamwambie ukweli.

Alihoji kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake ametumia neno ‘nimeambiwa’ kwa kiasi kikubwa, kwamba ingefaa mawaziri wake hasa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi; Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba wamwambie ukweli.
 
“Huyu huyu rais ndie aliwaambia wafanyakazi wakati wa mgomo wao kuwa akili za kuambiwa na viongozi wao wachanganye na za kwao, kwanini katika mambo aliyoambiwa na wasaidizi wake hakujiridhisha kwanza?” alihoji.
 
Hivi karibuni, Waziri Wassira aliwakejeli wapinzani kuwa wasitarajie tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala wa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013.
 
Alisema kuwa maandamano yaliyokuwa yanaandaliwa kumshinikiza rais asisaini muswada huo, hayana maana kwani rais hana sababu za kutousaini.
 
Licha ya Wassira kudai milango ya wapinzani kuzungumza na rais katika suala hilo imefungwa, Rais Kikwete amewasihi wapinzani wakae na serikali wajadili kasoro zilizopo kwenye muswada kama walivyofanya mwaka 2011 wakati mchakato unaanza hatua ya kwanza.
 
Hata Waziri Chikawe naye alimtisha rais hivi karibuni kuwa iwapo ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.
 
Lakini rais amewapuuza mawaziri wake hao na kutumia busara akisema kuhusu hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, saula hilo lilianzia bungeni hivyo linaweza kurudishwa huko lijadiliwe tena.

Kuhusu rais kumwandama Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu kuwa alisema uongo bungeni, Mnyika alisema hakufanya vema kumshambulia mbunge huyo kwani hayo hayakuwa mawazo yake binafsi bali maoni ya kambi ya upinzani.
 
“Inakuwa sio vizuri mbunge aliyetoa mawazo bungeni kwa mujibu wa katiba na kanuni za Bunge kushambuliwa kwa maneno makali na rais wakati alikuwa anatoa mawazo ya kambi wala si yake,” alisema Mnyika.

Lissu ajibu
Akizungumza na gazeti hili, Lissu amehoji hotuba ya Rais Kikwete iliyojaa neno “nimeambiwa” akisema ana uhakika gani wale waliomwambia kama hawakumdanganya?

“Maneno yaliyotajwa na rais kuhusu uteuzi wa wajumbe toka Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu, TEC na CCT yalizungumzwa kwenye kamati sio maneno yangu. Kikwete hakuwepo kwenye kamati, mimi nilikuwepo. Sasa mawaziri wake na wabunge wake wa CCM wamwambie ukweli, waache kumdanganya.

“Kikwete amesema mimi ni muongo, mnafiki, lakini hoja ambazo tulizipinga mfano ya ushiriki wa wadau wa Zanzibar, hata Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakari Khamisi naye ameniunga mkono. Je, na huyu ni mzushi, muongo na mfitini?” alihoji.

Aliongeza kuwa hoja ambayo rais anakimbilia kwamba alimzuia asiteue wajumbe 166, ilikuja bungeni mwaka 2011, wakaipinga, ikaondolewa. Lakini mwaka huu wameirejesha tena.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter