Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa muhimu wa mauaji ya mfanyabiashara bilionea wa Arusha Erasto Msuya wakati akijaribu kutoroka kwenda Burundi.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema mtuhumiwa huyo (jina tunalo), alikamatwa juzi asubuhi mkoani Kigoma akiwa katika harakati za kutoroka kuelekea nchi jirani ya Burundi.
Mtuhumiwa huyo ndiye anadaiwa kumshawishi marehemu kwenda kukutana na wauaji wake eneo la Mijohoroni wilayani Hai Agosti 7, mwaka huu na alikwenda pamoja na marehemu hadi eneo la tukio.
Habari zinadai mara baada ya marehemu kuuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka eneo la tukio akitumia moja kati ya pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo.
Tangu kutokea kwa mauaji hayo, polisi ambao wameonyesha weledi wa hali ya juu katika upelelezi wa mauaji hayo, walikuwa wakimfuatilia mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akijificha katika mikoa tofauti.
Habari nyingine zinadai kuwa watuhumiwa waliokodishwa kumuua mfanyabiashara huyo waliahidiwa kulipwa kitita cha Sh4 milioni kila mmoja na kila mmoja akalipwa malipo ya awali ya Sh1 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo aliyesema ni "muhimu" na kwamba mipango ya kumrejesha Moshi inaendelea kufanyika.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunafanya idadi ya watuhumiwa ambao wamekwishakamatwa hadi sasa kufikia wanane wakiwamo wafanyabiashara wawili wenye ukwasi ambao tayari wamefikishwa mahakamani
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....