WANAFUNZI WAKAMATWA WAKIFUKUA KABURI....!!

WATU watatu wakiwamo wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Sazila, wilayani hapa wamekamatwa wakiwa wanafukua kaburi la mtu aliyekufa mwaka 1938. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema lilitokea Mei 5 mwaka huu, saa 1:30 asubuhi, katika Kijiji cha Sazira, wilayani Bunda.

Kamanda Mwakyoma aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Deogratius Machunde (57), mkazi wa Ilemela jijini Mwanza, Rajabu Saleha (16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Sazira na Lucas Msilanga (19), ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Nyiendo iliyoko wilayani hapa.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwakyoma, watu hao walikamatwa na wananchi wa Kijiji cha Sazira wakifukua kaburi la marehemu Kigongo Makemba aliyefariki mwaka 1938.
Alisema marehemu alikuwa ni mganga maarufu wa jadi kijijini hapo na alipozikwa alizikwa akiwa amekalia kigoda.
Pamoja na Kamanda Mwakyoma kusema hayo, mjukuu wa marehemu huyo Kazimoto Kigongo, aliiambia MTANZANIA, kuwa watu hao walikamatwa wakiwa wameshafukua kaburi hilo, baada ya kufanya kazi hiyo kwa siku tatu.
“Watu hao waligunduliwa na wananchi ambao walitoa taarifa kwetu, kwamba kuna watu kila siku asubuhi wanakuja na kufukua kaburi.
“Baada ya kupata taarifa hizo, tuliweka mtego kwa kujificha vichakani karibu na eneo husika, ambapo baadaye watu hao walikuja na kuendelea kufukua kaburi hilo na ndipo tulipowazingira na kuwakamata wakiwa na majembe, koleo, sururu, nyundo, futi za kupimia pamoja na udi.
“Tulipowahoji walisema walikuwa wanafukua madini aina ya mercury, yaliyowekwa na Wajerumani katika eneo hilo,” alisema.
Taarifa zilizotukifikia wakati tunakwenda mitamboni kupitia kwa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Masoud Mohamed, zinasema kuwa, watuhumiwa hao, walifikishwa mahakamani hapo juzi mbele ya Hakimu, Safina Simufukwe.
Alisema waliposomewa mashitaka yao, walikana kosa na kurudishwa mahabusu hadi Mei 21 mwaka huu, kesi yao itakapoendelea tena.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter