HUJAFA Hujaumbika, kiungo wa Azam FC, Ibrahim Bakari ‘Jeba’, hataweza kucheza soka tena baada ya kuzuiwa na madaktari.
Madaktari mahiri wa nchini India wamechukua uamuzi huo baada ya kumfanyia vipimo na kugundua kuwa ana tatizo kwenye ini.
Jeba ambaye mashabiki wa soka nchini humfananisha na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’, wakati fulani alitaka kusajiliwa Simba lakini wakashindwa kuelewana na Azam FC ambao walikanusha taarifa za usajili huo na kusema bado wana mkataba naye wa miaka miwili.
Jeba ambaye hajafikisha miaka 25, hatacheza soka tena kama ilivyokuwa kwa kiungo Fabrice Muamba wa Bolton ambaye alianguka uwanjani na mwisho madaktari wakapitisha uamuzi astaafu mpira.
Mmoja wa mabosi wa Azam ameliambia Championi Ijumaa kuwa, kiungo huyo aligundulika na matatizo ya ini baada ya klabu hiyo kumpeleka nchini India miezi mitatu iliyopita alipokuwa akikabiliwa na matatizo ya goti.
“Baada ya kugundulika na ugonjwa wa Hepatitis B ambao ulishambulia ini lake, ikashindikana hata kumfanyia upasuaji wa goti lake tena. Akapewa dawa na kurudi nchini na alipomaliza hizo dawa alikwenda tena kufanya uchunguzi hapa Tanzania katika Hospitali ya Aga Khan, akajibiwa kweli anaugua ugonjwa huo, hawezi kucheza soka tena na sasa yupo kwao Zanzibar,” alisema bosi huyo.
Alipoulizwa juu ya mchezaji huyo, Kocha wa Azam, Stewart Hall alikiri kuwa Jeba ni mgonjwa lakini hakutaka kufafanua kiundani akidai watafutwe viongozi wa klabu.
Ugonjwa wa Hepatitis B unasambazwa na virusi vinavyofahamika kwa jina la Hepatitis B Virus (HBV).
Akizungumzia suala hilo, daktari wa timu hiyo ambaye ni mkongwe katika masuala ya michezo, Mwanandi Mwankemwa alikiri kuumwa kwa kiungo huyo.
“Anahitajika kupumzika kwa muda mrefu lakini pia anatakiwa asifanye mazoezi magumu kitu ambacho katika soka ni kigumu, sasa anatumia dawa lakini kuhusu hilo la kuweza kucheza tena soka sidhani kama litakuwa rahisi kulingana na madhara ya ugonjwa wenyewe,” alisema Mwankemwa.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....