Kijana aliyemkimbiza hadi kumkamata mtu anayedaiwa kuhusika na kulipua bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha akiwaelezea wananchi ilivyokuwa.
ALIYEMKIMBIZA hadi kumkamata mtu anayedaiwa kuhusika na kulipua bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha Jumapili iliyopita na kuua watu 3 na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa ameibuka.
Kijana huyo ambaye wakati akizungumza na watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari jijini Arusha juzi alisahau kutaja jina lake, alisema kuwa shughuli ya kumnasa mtuhumiwa huyo haikuwa lelemama hata kidogo.Alisema siku ya tukio baada ya bomu hilo kulipuliwa kanisani hapo, yeye alimwona mlipuaji huyo hivyo akaungana na watu wengine kumkimbiza.
“Mtuhumiwa alikuwa akikimbia ujue, sisi tulimkimbiza bila kuogopa kama ana mabomu mengine kwenye mfuko. Alipoona hatukati tamaa, alifika kwenye shamba la miwa akajilaza, lakini mbwa waliokuwa na sisi walitusaidia sana,” alisema shujaa huyo.
Aliendelea kusema kuwa walipomdaka mtuhumiwa huyo walimkuta na mfuko wa rambo, walipochungulia ndani yake walishtuka, kumbe alikuwa na mabomu yaliyosalia!
Hata hivyo, alisema yeye na mabomu yake hawakumwachia na dakika chache wananchi wenye hasira kali walifika eneo hilo wakiwa na silaha za jadi wakitaka kumuua ndipo polisi walipofika eneo hilo na kumchukua mtuhumiwa huyo kwenda naye kituoni.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kijana huyo amekuwa staa ghafla, hivyo wakaitaka serikali kumfikiria kwani ameonesha kitendo cha kishujaa.
“Huyu kijana amekuwa staa ghafla aisee, kitendo alichokifanya ni cha kishujaa, si rahisi, serikali ingemfikiria kwa lolote,” alisema mtu mmoja aliyejiita Massawe na kuungwa mkono na wenzake.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....