Shahidi aeleza alivyoombwa rushwa na daktari Muhimbili..!!


Deodata MatikoDaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
Kitengo cha Mifupa (Moi), 

Shahidi Stanford Mhina, katika kesi inayomkabili daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Mifupa (Moi), Deodata Matiko, kuomba rushwa kwa mgonjwa, amedai mahakamani kwamba muuguzi Erick Kimwomwe, alimwomba rushwa ya Shilingi milioni moja ili mgonjwa wake apate tiba ya haraka.

Kadhalika, shahidi huyo amedai mahakamani jinsi alivyofanikisha mtego wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hadi mshtakiwa akanaswa.

Mhina, alitoa madai hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa.
Shahidi huyo ambaye alikuwa akimuuguza ndugu yake hospitalini hapo, alidai muuguzi Kimwomwe, alimwomba rushwa ya Shilingi milioni moja akampe daktari ili akamfanyie haraka upasuaji ndugu yake aliyekuwa amelazwa Jengo la Sewahaji, wodi namba 18, akisumbuliwa na mgongo.
Mgonjwa huyo, Fanuel Gideon, alipelekwa Moi baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Gideon, alipata ajali ya gari maeneo ya Kibaha na kuvunjika mgongo.

“Niliwafahamisha maofisa wa Takukuru, Leonard Mkama, Patrick Katemba, Lina Mazengo na Anjela, tukaondoka hadi Muhimbili wakidai wanataka kumuona mgonjwa, wakati tukijiandaa kuingia wodini, tulikutana na Erick mlangoni...nilimtambulisha Erick kwa Mazengo kwamba ni shemeji yangu, akaniuliza, vipi kaka, nikamjibu wewe tu, akaniambia nikamuone saa nane, mapokezi Moi” alidai shahidi na kuongeza:

“Mimi na maofisa wa Takukuru, tuliingia kumuona mgonjwa, tulipotoka waliniambia watasubiri hadi saa nane ninapokwenda kukutana na Kimwomwe, kwa ajili ya kumpa fedha za rushwa kama tulivyokubaliana,” alidai Mhina.

Alidai ilipofika saa 8:00, aliongozana na Mazengo hadi mapokezi Moi, akapiga simu kumwita Erick, alipofika aliwachukua hadi ghorofa ya kwanza chumba namba tatu.

“Wakati tukielekea katika chumba hicho, maofisa wengine wa Takukuru walikuwa wakitufuatilia bila muuguzi huyo kujua, tulipofika mlangoni, Kimwomwe aligonga mlango tukaingia ndani…nilimkuta binti kavaa koti jeupe nikajua ndiye daktari, nilipouliza daktari wenyewe yupi, yule binti akajibu katoka isipokuwa kamwachia maagizo amchukulie mzigo wake,” alidai shahidi huyo.

“Ofisa wa Takukuru aliniamuru niwape fedha, nikaziweka mezani, daktari na Kimwomwe, walishirikiana kuhesabu fedha hizo, zilipofika Sh. 300,000, daktari alimshtukia ofisa huyo na kumwambia mbona unachezea simu usijekuwa umeleta fedha za moto,” alidai shahidi huyo akimnukuu mshtakiwa.

Hata hivyo, ofisa huyo wa Takukuru alimjibu kwamba anachezea simu kwa kuwa ni mambo ya `blackberry', walipoendelea kuhesabu maofisa wengine waliingia na kuwakamata washtakiwa ambao baadaye walifikishwa mahakamani.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter