Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wanafamilia, hali ya mbunge huyo si nzuri kwani pamoja na kulazwa Aga Khan, alishauriwa na madaktari kwenda India kwa matibabu zaidi ila Bunge limechelewesha safari hiyo kwa siku kumi tangu ushauri huo ulipotolewa. Akizungumza na gazeti hili jana, mdogo wa mbunge huyo, Tundu Lissu, alisema dada yake alitoka hospitalini jana mchana.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), alisema kuwa madaktari walimweleza mgonjwa wao kuwa hana sababu ya kuendelea kubakia hospitalini akisubiri safari ya India. “Walimshauri akasubirie nyumbani, ingawa hali yake sio nzuri,” alisema Lissu.
Alipoulizwa kama taratibu za kumpeleka India zimefanyika au la, Lissu alisema zilipaswa kuwa za kibunge lakini wamecheleweshwa sana na sasa wanataka kuchukua jukumu hilo kama familia ili impeleke akapate matibabu. Lissu aliongeza kuwa alipowasiliana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ili kujua msimamo wa ofisi yake, tangu juzi alikuwa akiahidiwa kuwa angempigia kumweleza utaratibu, lakini hadi jana alikuwa hajapigiwa.
Tanzania Daima iliwasiliana na Dk. Kashililah kuhusu suala hilo, ambapo alikiri mbunge huyo kuumwa na kudai kuwa alikuwa njiani kwenda kumjulia hali. Alipoulizwa kama kuna utaratibu wa kumsafirisha kumpeleka India kwa matibabu zaidi, Dk. Kashilillah alisema;
“Mbona unaniuliza hivyo kwani wewe umeshajua ugonjwa anaoumwa hadi uniulize hivyo? Sisi tunafuata ushauri wa madaktari, wakisema tumpeleke tutafanya vile, wao ndio wanaamua.”
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....