Katika tangazo hilo (ambalo limepachikwa hapo chini) mwanamke mmoja anamwuliza mwenziye kuhusu mahusiano yake na mumewe na kujibiwa kuwa mume amekuwa mlevi siku za hivi karibuni na anashinda kilabuni.
Tangazo linaendelea ambapo mwulizaji anauliza kuhusu “mpango wa kando” (hawara) ambapo anayeulizwa anamkodolea macho hawara yake aliye katika meza nyingine akiendelea na biashara ya kuuza matunda, huku akisema “anaridhishwa” naye, hata ikiwa hapati muda mwingi wa kuwa naye.
Ndipo mwuliza swali anauliza endapo wawili hao wanatumia condom, ambapo kwa aibu, anayeulizwa anazubaa kimya.
Karibu na mwisho wa tangazo hilo anasikika shoga akimshauri mwenziye juu ya umuhimu wa kutumia condom ili kujilinda yeye na wale anaowapenda, na kuisha kwa binti anayeonekana kuvalia sare ya shule, akimkimbilia mama na kumkumbatia, kisha linatamatia kwa maneno, “Weka Condom Mpangoni”.
Viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam wamesema sababu ya kulipinga tangazo hilo ni kwa kuwa linachochea “mpango wa kando” (usaliti katika ndoa na mahusiano), uzinzi na ngono kabla ya umri (uasherati) badala ya kusisitiza juu ya ngono salama ili kukabiliana na maambuki za VVU/UKIMWI.
Wakailaumu tume ya mawasiliano nchini humo (CCK) kwa kushindwa kulichuja tangazo hilo.
Afisa Afya wa Kenya (Kenya National AIDS and STI Control Programme) Dr Peter Cherutich amesema sababu ya kuweka tangazo lenye maudhui hayo linatokana na takwimu zinazoonesha kwamba asilimia 30 ya wanandoa wanajihusisha na “mpango wa kando” (ngono nje ya ndoa zao) na wengi wao hawatumii condom.
Takwimu za shirila la Umoja wa Mataifa linalohusika na HIV/AIDS linaonesha kuwa takriban watu milioni 1.6 kati ya watu wote milioni 41.6 nchini Kenya wanaishi na VVU/UKIMWI.
Viongozi wa dini pamoja na Wazazi wamesisitiza kuwa hata muda wa kuonekana kwa tangazo hilo siyo muafaka kwani hutokea dakika chache tu kabla ya kusomwa kwa taarifa ya habari kwenye televisheni ya Taifa, muda ambapo mara nyingi familia zinakuwa zimejumuika kutizama televisheni, jambo ambalo linawatia aibu mbele za watoto wao kiasi cha kubadili chaneli ili kuepusha soni.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....