Madereva Wa Maroli Ya Mizigo Kupima VVU Wakiwa Safarini

 
 

 MADEREVA wa maroli ya mizigo na kwenda mikoani na nchi jirani sasa watakuwa hawana shida ya kupata maarifa, elimu na hudumu mbali mbali za Virusi vya UKIMWI—ikiwa ni pamoja na kupima kwa hiari ili kujua hali zao—kutokana na ufunguzi wa kituo cha maarifa ya udhibiti wa ugonjwa huo katika eneo la Mdaula, nje kidogo ya mji wa Chalinze, Mkoa wa Pwani.
 
Uzinduzi huo uliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw. Ahmed Kipozi pamoja na viongozi mbalimbali wa wilaya na vijiji vya Mdaula, Matuli na Mbena.
 
Huduma zitakazotolewa na kituo hicho ambacho kimejengwa kwa gharama ya Sh. 57 milioni ikiwa ni mchango wa Mradi wa Kudhibiti UKIMWI Eneo la Maziwa Makuu (GLIA) kupitia TACAIDS pamoja na mchango wa wanajamii wa Mdaula na Halmashauri ya Bagamoyo kwa kutoa wataalam wakati wa ujenzi, ni pamoja na ushauri nasaha na upimaji nasaha wa VVU.
 
Nyingine ni kutoa elimu na maarifa mbalimbali za UKIMWI, burudani kwa jamii kama vile luninga, michezo ya darts na pool pamoja na huduma za intaneti.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mrisho alisema uzinduzi huo ulikuwa unabainisha nia ya serikali ya kuleta huduma za jamii ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na vita dhidi ya UKIMWI karibu na wananchi.
 
“Nia ya serikali ni kuhakikisha huduma zinafika karibu na kaya. Kwa mfano, wananchi hawapaswi kuendelea kwenda mbali kufuata huduma za tiba, matunzo, upimaji au elimu kuhusu UKIMWI. Badala yake huduma hizi ndizo ziwafuate ili kuwapunguzia mzigo wa safari na usumbufu. Na hiki ndicho kimefanyika hapa siku ya leo,” alisema Dk. Mrisho.
 
Akasema, pamoja na kuwa kituo hicho kimejengwa ili kuwapa uwepesi madereva wa malori na magari makubwa ya mizigo yaendayo mikoani na nchi ya jirani kuweza kupata huduma mbali mbali na maarifa ya jinsi ya kupambana na VVU pamoja na UKIMWI, wakazi wa Mdaula pamoja na vijiji jirani nao pia watanufaika na kituo hicho.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter