Mwanafunzi azuiwa kufanya mtihani kutokana na ujauzito


MWANAFUNZI Agnes Vedasto (17) amezuiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidacho cha nne Sekondari ya Bukoba, kutokana na kudaiwa kuwa na mimba inayokaribia miezi tisa.
Agnes mwenye namba ya mtihani S.0304/0003 alizuiwa na Ofisa Elimu Taaluma, Christina Shadrack na Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu, Wandele Pamba wote wa Manispaa ya Bukoba waliofika shuleni hapo kwa lengo la kusambaza vifaa.
Inadaiwa kuwa baada ya maofisa elimu hao kufika shuleni kabla ya wanafunzi kuingia darasani kuanza kufanya mtihani, waliulizwa na Mkuu wa shule, Deus Gasper kama mwanafunzi huyo aliyefika jana asubuhi kwa lengo la kufanya mtihani, anaweza kuruhusiwa kutimiza.
Baada ya kuzuiwa kuingia chumba cha mtihani, mwanafuanzi huyo alilazimika kurejea nyumbani eneo la Hamugembe, Manispaa ya Bukoba.
Mkuu wa Sekondari ya Bukoba, Gasper alisema kwa miezi mitatu mwanafunzi huyo  alikuwa haonekani shuleni na uongozi wa shule ulitambua ni mjamzito, mzazi wake aliitwa na kukiri  kuwa mwanae ana mimba.
Gasper alisema wakati anatambuliwa jina lake tayari lilikuwa limeshapelekwa Baraza la Mitihani na liliporudi alitaarifiwa na wanafunzi wenzake , akaamua kufika kwa lengo la kufanya mtihini wa kuhitimu kidato cha nne akiwa amevaa sare na vifaa vyote vya shule.
Ofisa Elimu Manispaa ya Bukoba, Simon Mwombeki alisema kwa mujibu wa sheria ya elimu namba 25, ni kosa mwanafunzi kupata ujauzito akiwa shule, kuoa wala kuolewa, hivyo mwanafunzi huyo tayari amekosa sifa.
“Mama yake mzazi (hakumtaja jina) jana alifika ofisini kwangu na kuniomba mtoto wake  aruhusiwe kufanya mtihani, lakini nilishindwa jinsi ya nimsaidie,” alisema Mwombeki.
Mwombeki alisema kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mama mzazi, mtoto wake anatarajiwa kujifungua kati ya Oktoba 25 na 26, mwaka huu.
Mapema mwezi uliopita mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kabirizi, wilayani Muleba, Happiness Mzalendo (18) alijifungua mtoto wa kiume baada ya kuumwa uchungu akiwa katika chumba cha mtihani.
Mwanafunzi huyo alilamizika kuomba msaada kwa msimamizi wa mtihani ambaye alimtoa nje ya chumba na kujifungulia chini ya mgomba ulioko katika shamba la shule.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter