Kenya yaiomba radhi Tanzania....yasema ilifanya kosa kosa kubwa kuibagua Tanzania ambayo ndio Mwanzilishi wa EAC



 
SIKU nne tangu Rais Jakaya Kikwete alihutubie Bunge na kuweka bayana msimamo wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Kenya imempongeza huku ikisisitiza kuwa nayo itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu. 
 
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa na hatua ya marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame wa Rwanda kuanza mazungumzo ya kuitenga Tanzania, lakini akasema kamwe haitaondoka kwenye jumuiya hiyo.
 
Alisema nchi hizo zimeanza mazungumzo kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta, jambo linalovunja misingi ya jumuiya hiyo.
 
Kufuatia kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jana alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed.
 
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Membe alisema Kenya imesema kuwa mazungumzo kati yake na nchi za Uganda na Rwanda kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta yalifanyika bila nchi yake kujua kwamba inavunja misingi ya jumuiya.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya yuko nchini, ametumwa na rais wake, Uhuru Kenyatta kuja kutoa pongezi kwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa bungeni,” alisema Membe.
 
Kwa mujibu wa Membe, Kenya ilidai kuwa ilifanya hivyo bila kufahamu kwamba nchi hizo zinaibagua Tanzania ambayo ni mwanzilishi wa jumuiya hiyo.
 
Tunapongeza hotuba ya Rais Kikwete bungeni na kuahidi kwamba Kenya itaendelea kuwa mwanachama imara wa jumuiya hiyo, atakayelinda misingi imara na taratibu zilizowekwa,” alisema Membe akimkariri Waziri wa Kenya.
 
Aliongeza kuwa ujumbe huo ulikiri kutokea kwa tatizo hilo, hasa ikizingatiwa kwamba viongozi wa nchi hiyo wamechukua madaraka Aprili 8, mwaka huu.
 
Kwa ujumla Kenya inasema ilipotoka kufanya mazungumzo kuhusu mambo ambayo yapo kwenye mkataba bila kuishirikisha Tanzania, alisema.
  
Aidha, Mhe. Mohammed alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika  kuiunga mkono nchi yake katika kesi inayowakabili Rais na Makamu wa Rais wan chi hiyo huko Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Alieleza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono kesi hiyo iahirishwe hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi hao kuwatumikia wananchi waliowachagua.

Tunaishukuru sana Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Kenya katika suala linalowakabili  viongozi wetu la  kushitakiwa ICC. Tumaamini kabisa kuwa hatuwezi kumaliza kesi hiyo wala kupata kibali (deferral) cha kesi hiyo kusogezwa mbele bila kuungwa mkono na nchi kama Tanzania” alisisitiza Mhe. Mohammed.

Awali akimkaribisha Bibi Mohammed kuzungumza na Waandishi wa Habari, Mhe. Membe alisema kuwa Serikali ya Tanzania imefurahishwa sana na ziara  ya Ujumbe huo mzito kutoka Kenya na Tanzania inazipokea kwa mikono miwili pongezi hizo za Kenya kwa Rais Kikwete na kwa Watanzania kwa ujumla. 

Kuhusu suala la viongozi wa Kenya kupelekwa ICC, Mhe. Membe alisema kuwa, Tanzania bado inaunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuahirisha kesi hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapa nafasi Viongozi hao kukamilisha baadhi ya mambo waliyojipangia kuyatekeleza kwa  nchi yao.

“Tunashukuru Mwendesha Mashitaka wa ICC ametoa tamko la dharura kwa kesi dhidi ya Rais Kenyatta kuanza kusikilizwa tarehe 5 Februari, 2014 badala ya tarehe 12 Desemba, 2013. Hata hivyo bado tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusogeza mbele kesi hiyo kwa mwaka mmoja hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi hawa kuitumikia nchi yao kikamilifu kwani tunaamini katika kipindi hicho Serikali ya Kenya itakamilisha mengi” alisisitiza Mhe.  Membe.

Mhe. Membe aliongeza kuwa, kulingana na kauli ya Mhe. Mohammed alipozungumza nae, migogoro ya Kenya iliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 imetatuliwa kwa asilimia 75, ambapo baadhi  ya wahusika wamepatiwa ardhi, watuhumiwa wamepelekwa mahakamani na baadhi yao wamepewa fidia kutokana na madhara mbalimbali waliyoyapata. 
 “Tanzania ipo pamoja na Kenya na ipo kuhakikisha Serikali hiyo inatawalika kwa kuwapa nafasi viongozi waliochaguliwa na wananchi kuongoza”, alisema Mhe. Membe.

Mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed ulifanyika jana  katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali zote mbili..
 
Nchi za Uganda na Rwanda bado hazijasema chochote kuhusiana na hotuba hiyo ya Rais Kikwete.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter