MAPAPARAZI wetu bado wapo katika zoezi la kufuatilia uadilifu wa mastaa, maadiili ya kazi za jamii na usalama wa viongozi mbalimbali wa serikali.
Shamsi Vuai Nahodha.
Baada ya siku chache nyuma kuwanasa mastaa wa kike kwenye mtego wa wanaojiuza sanjari na kumbamba daktari mmoja akitaka kufanya jaribio haramu la kutoa mimba ya paparazi ambaye alijifanya mchumba wa mtu, wiki hii zoezi lilihamia serikalini.Mapaparazi walifanya zoezi la kuhakiki usalama wa mawaziri kama upo imara au ni wa kusuasua. Hiyo yote ilitokana na ukweli kwamba, wapo mawaziri kwa nafasi zao za kikazi wanatakiwa kulindwa sana.
Ilikuwa Jumanne iliyopita, majira ya mchana, mapaparazi walitia timu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha.
Yeye kama waziri mwenye dhamana ya ulinzi wa taifa, mapaparazi walitaka kujua kama ulinzi huo unaanzia kwake mwenyewe au la!
Awali ya yote, mapaparazi wetu walikwenda Kariakoo kwenye maduka yanayouzwa silaha za bandia ‘toi’, ikiwemo bastola na kujinunulia moja kwa ajili ya matumizi kisha kushika njia kuelekea kwenye wizara yake Upanga, jijini Dar es Salaam ili kujaribu kupita na ‘bastola’ hiyo mpaka kwa waziri.
Kabla ya kuingia getini, paparazi mmoja aliitumbukiza bastola hiyo kwenye sehemu ya juu ya suruali upande wa kulia na kuchomoa shati ili isionekane.
Walinzi waliokuwa getini muda huo waliwazuia mapaparazi kwenda kwa waziri hadi wajieleze walikuwa akina nani na walikuwa na shida gani.
Mkuu wa msafara wa mapaparazi aliwaambia wao ni waandishi wa habari walikuwa na shida ya kuonana na waziri huyo.
Baada ya mawasiliano kati ya getini na ofisi ya waziri, mapaparazi hao waliokuwa watatu walikubaliwa kupita lakini kwa sharti la kusachiwa kwanza kwa mikono ili ulinzi ujiridhishe kwamba hawakuwa na kitu cha kuweza kumdhuru mheshimiwa waziri.
Mlinzi alipofika kwa paparazi mwenye ‘bastola’ alianza kwa kumshika sehemu nyingine za mwili kama mifuko ya nyuma, mbele, kwenye shati na kumalizia mwilini na ndipo alipokumbana na ‘silaha’ hiyo.
“Hii nini?” aliuliza mlinzi huyo huku amemkazia macho paparazi.
“Hii ni toi la bastola, nimemnunulia mtoto wangu.”
Mlinzi: Utaliacha hapa, ukitoka kwa waziri ndiyo utalichukua.
Paparazi: Sawa.
Hata hivyo, walinzi hao walionesha kudhibiti vitu vingi vya mapaparazo hao ikiwemo kamera kubwa.
Baada ya mapaparazi kufika kwa waziri na baada ya salamu walimuomba mheshimiwa huyo wapewe japo kamera tu jambo ambalo waziri alilifanya kwa kupiga simu mapokezi. Kuhusu bastola yao feki waliipata baada ya kutoka kwa Mheshimiwa Nahodha.
Tunatoa pongezi kwa walinzi waliokuwepo getini siku hiyo kwani kitendo chao kimeonesha ni jinsi gani waziri huyo analindwa kwa usahihi.
Hata hivyo, Mapaparazi wetu wapo kazini wakiendelea kufuatilia ulegevu sehemu za kazi, hasa serikalini.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....