Na Eliasa Ally, Iringa
BIBI kikongwe Sabina Kigonole (70), mkazi wa Kitongoji cha Msali katika Kijiji cha Ilawa, wilayani Kilolo, Iringa ameuawa kinyama baada ya kukatwa kwa mapanga kichwani na miguuni na vijana wawili, Kelvin Madati (22) na Edgar Madati (20) ambao ni wajukuu zake.
Bibi kizee huyo ameuawa na wajukuu zake hao wakimtuhumu kuwa ni mshirikina ambapo wanadai amewaloga ili wasipate maendeleo yao binafsi na kuendelea kubakia masikini katika maisha yao.
Akizungumzia mauaji ya kikongwe huyo wiki iliyopita ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema kuwa mauaji hayo yalitokea Februari 17, saa 9:15 usiku wa manane baada ya vijana hao kumvamia bibi yao huyo na kumkatakata mapanga akiwa amelala nyumbani kwake.
“Walikuwa wakimtuhumu bibi yao kuwa ni mchawi na ndiye anayewaloga ili wasipate maendeleo na baada ya kufanya unyama huo wametokomea kusikojulikana na jeshi la polisi mkoani Iringa linawatafuta,” alisema Kamuhanda.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita akizungumzia kuuawa kinyama kwa bibi huyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa waachane na kuendekeza imani potofu za ushirikina.
“Serikali haitakubali kuona mauaji ya kinyama yanaendelea baina ya wananchi, kama waliofanya vitendo hivyo vya kinyama ni wajukuu halisi wa kikongwe aliyeuawa, kwa nini asingewaloga na kuwaua wakiwa wadogo hawajitambui, tutahakikisha tabia hizi zinakomeshwa,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....