Polisi Wazima Maandamano Lindi, Mtwara napo Hakukaliki...!!

Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kikiwa kazini (picha hii haina uhusiano na maandamano ya Mtwara)
HALI ya usalama mkoani Mtwara bado tete baada ya jana Jeshi la Polisi kuwahamishia mkoani Lindi waandishi wa habari 150, waliokuwa katika mkutano wa siku tatu wa Kongamano la Nane la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliofanyika Mtwara.
Waandishi hao walitoroshwa na polisi jana saa 11:00 alfajiri kwenda mkoani Lindi ambapo pia polisi walifanikiwa kusitisha maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), kwa lengo la kutaka kupata tathmini ya mwendelezo wa miradi ya gesi na maji.
Habari zinasema wananchi hao walitaka kuwateka waandishi wa habari kwa madai kuwa waliandika habari za kuzimwa kwa uasi wao kuhusu gesi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jambo wanalodai siyo kweli.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hata hivyo, alisema kuwa taarifa hizo zilikuwa ni tetesi tu, akiongeza kwamba katika Mkoa wa Lindi kulikuwa na taarifa kwamba yangefanyika maandamano makubwa, lakini hakuna kilichotokea.
“Ulikuwa ni uvumi wa watu, unajua hivi sasa anaweza kuibuka mtu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuhusu jambo lolote tu, ila suala hilo la waandishi wa habari ni kweli na asubuhi niliambiwa na OCD, lakini hali ni shwari sasa,” alisema.
Mgogoro wa gesi uliibuka mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Serikali kutangaza mpango wake wa kutandaza bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi wa mkoa huo walipinga mpango huo huku wakiungwa mkono na watu wa kada mbalimbali nchini, vikiwamo vyama vya siasa.
Katika kuonyesha kutotaka gesi itoke mkoani humo, wananchi hao walifanya maandamano, sambamba na kuchoma moto nyumba za baadhi ya wabunge, ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jengo la Mahakama ya Mwanzo Mtwara.
Januari 29 mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alizungumza na wananchi wa mkoa huo na kuwatuliza jazba, baada ya kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.
Pinda alisema kuwa hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirishwa kwa njia ya bomba na kueleza kwamba kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa katika Kijiji cha Madimba, mkoani humo na mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda ilipingwa na wananchi wengi ambao walidai kuwa imejaa siasa, ndiyo chanzo cha wananchi hao kutaka kuwateka waandishi wa habari kwa maelezo kuwa waliandika habari zenye kichwa cha habari ‘Pinda azima uasi Mtwara’, jambo ambalo walisema siyo kweli.

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA....

 

Copyright © 2010 GUMZO LA JIJI.

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter